March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

wabunifu 200 watambuliwa,sh.2.3bilioni zatumika kuwaendeleza

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imesema tayari imewatambua wabunifu 200 ambao bunifu zao zilifanya vizuri katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) katika miaka iliyopita ambapo jumla sh.bilioni 2.3 zimetumika kwa ajili ya kusapoti bunifu hizo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Eliamani Sedoyeka  wakati akifungua warsha kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma iliyolenga kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala ya ubunifu ili waweze kuelimisha umma kuhusiana na Maonyesho ya MAKISATU ya mwaka huu yanayoatarajia kuanza Mei 15-Mei 20 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Aidha amesema,katika mwaka wa fedha unaoisha Juni mwaka huu serikali ilitenga sh.Bilioni moja katika eneo la ubunifu huku kwa mwaka ujao wa fedha eneo hilo likitengewa kiasi cha sh. bilioni 5.5 .

Profesa Sedoyeka amesema kiasi hicho cha fedha kinatengwa kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya kubuni na kuendeleza bunifu na kuzijengea uwezo taasisi au mbunifu mmoja mmoja ili bunifu zao  ziweze kuingia sokoni.

“Katika  mwaka wa 2022/23 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 5.5 katika masuala ya ubunifu kwa lengo la  kuhakikisha wanaboresha mashindano hayo pamoja na bunifu zinazotengenezwa na watanzania.”amesema

Amesema zawadi  za washindi katika mashindao ya MAKISATU mwaka huu ni shilingi milioni tano  kwa mshindi wa kwanza ,mshindi wa pili shilingi milioni tatu,huku mshindi wa tatu akipata kiasi cha shilingi milioni mbili.

Aidha alisema,wale watakaoingia fainali ya mashindano hayo watapata fursa ya bunifu zao kuendelezwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sayansi,Teknolojia na Ubunfu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Maulilio Kipanyula amesema jumla ya wabunifu 862 wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho hayo kutoka katika makundi saba.

Akitoa neno la shukrani kwa  niaba ya wanahabari waliopata mafunzo hayo ambaye pia ni Balozi wa Mazingira Sakina AbdulMasoud alisema,watayatumia mafunzo hayo kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya ubunifu.

Aidha amewaasa wanahabari kukumbuka kuelimisha wabunifu kuhusiana na masuala ya utunzaji wa mazingira  pindi wanapotengeneza bunifu zao.

Maonyesho ya MAKISATU mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo’ubunifu kwa Maendeleo enedelevu.’