April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi akabidhi sh.laki tano ujenzi nyumba ya Katibu UWT Chunya

Na Esther Macha ,Timesmajira,Online,Chunya

MBUNGE wa Viti Maalum  Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji mhandisi ,Maryprisca Mahundi amekabidhi  shilingi  laki tano (5)kwa ajili ya  ujenzi wa nyumba ya Katibu  wa umoja wa wanawake wilaya ya Chunya UWT.

Mhandisi Mahundi amesema kuwa mwaka jana alipotembelea eneo la ujenzi wa nyumba ya Katibu katika maeneo ya Mbughani aliweza kuchangia mil.5  ambazo zilifyatua tofari  na usombaji  wa mawe ya Msingi.

Aidha Mhandisi Mahundi amesema kuwa huo ni mwanzo katika kuhakikisha katibu anaishi kwenye makazi bora.

“Kipindi cha mwaka jana niliwazesha  wanawake  mitaji  na majiko  ya gasi ili kutunza  vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira “amesema 

Hata hivyo Mhandisi Mahundi amesema kuwa mpaka sasa vifaa vyote vya ujenzi vimekamilika  na kwamba nyumba hiyo ya katibu itakuwa mfano kwa mkoa wa Mbeya .

“Tumeanza mambo ya maendeleo  kwa kasi kubwa na hapa yatakuja mazuri zaidi  ya haya tulitoa ahadi lazima tutekeleze ,nashukuru wadau wanaoendelea kuniunga mkono katika ujenzi huu “amesema Mhandisi Mahundi.

Kwa upande wake Katibu wa umoja wa wanawake wilaya ya Chunya (Uwt)Zaitun Sembo amesema kuwa pamoja na nguvu ya mhandisi Mahundi ya ujenzi wa nyumba hiyo bado kuna  changamoto ya  mahitaji ya fedha  kushindwa kuendelea na ujenzi  huku wadau waliotoa ahadi za kuchangia ujenzi huo kushindwa kukamilisha ahadi zao.

Sembo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa nyumba hiyo umegharimu  shilingi Mil.7.

Jokeli Selemani ni Katibu wa chama cha mapinduzi Wilaya ya Chunya amesema kwamba mbunge huyo amekuwa kinara wa maendeleo kwa wanawake wa wilaya hiyo  kutokana na kugawa majiko ya gesi pia kufuatia mpango ulioanzishwa na  CCM taifa wa ujenzi wa nyumba za makatibu wa chama nchini kote kiongozi huyo amewezesha kuanza kwa ujenzi huo.

Amesema kuwa nyumba nyingi za makatibu  hazina ubora zilizopo ni vituko  hazina hadhi.

Mmoja wa wanachama wa chama mapinduzi ambaye ni Diwani wa vitimaalum kata ya Makongorosi ,Sophia Mwanautwa amesema ujenzi huo wa nyumba ya katibu ni hatua nzuri na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na mbunge wa vitimaalum na Naibu waziri wa maji mhandisi Mahundi.

“Tunahitaji viongozi wa mfano kama hawa  ambao hawaoni kazi kujitoa ,tunazidi kumwombea kiongozi wetu  jambo aliloanzisha likamilike zaidi ya zaidi”amesema.