April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NDEJEMBI:Taasisi zinazokiuka sheria ya Serikali Mtandao zisifumbiwe macho

Na Mwandishi wetu Timesmajira online,Dodoma
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi ameiagiza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuzichukulia hatua stahiki taasisi zote za umma zinazokiuka matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma alipokuwa akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichohusu mafunzo ya uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za Serikali Mtandao.

Amesema e-GA ni mamlaka kamili hivyo, inapaswa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria pale inapoona taasisi za umma zinajenga mifumo ya TEHAMA bila kibali cha mamlaka hiyo au zinapokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Serikali Mtandao.

“e-GA mna meno kisheria hivyo anzeni kuitekeleza Sheria ya Serikali Mtandao kwa vitendo kwa kuzichukulia hatua mara moja taasisi zote zinakwenda kinyume na sheria hiyo,” amesisitiza Ndejembi

Akizungumzia malalamiko ya upatikanaji wa mtandao kwenye baadhi ya maeneo, Ndejembi amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ambayo wananchi wamekuwa wakiilalamikia pindi wanapohitaji huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma kupitia mifumo ya TEHAMA.

“Unakuta mwananchi anatembea umbali mrefu kufuata huduma ya kulipa kodi kwa manufaa ya taifa, halafu anaambiwa mtandao hakuna kwani mfumo haufanyi kazi, na wakati mwingine kwenye halmashauri zetu kutengeneza namba ya malipo mwananchi anaambiwa mtandao uko chini jambo ambalo linakwamisha utoaji wa huduma,” amesema na kuongeza kuwa

” Serikali ya Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuwa na Serikali ya Kidijitali itakayoondoa changamoto ya wananchi kutopata huduma bora na kwa wakati, hivyo amewaasa wataalam wa TEHAMA kutumia ujuzi wao katika kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji wa huduma Serikalini.”

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge amesema, kikao kazi hicho cha wataalam wa TEHAMA kinadhihirisha dhamira ya ofisi yake kupitia mamlaka ya Serikali Mtandao kuwa na jukwaa la kudumu la kukumbushana mkakati wa kuhakikisha TEHAMA inatumika ipasavyo kurahisisha utendaji kazi wa  taasisi za Serikali kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amemhakikishia Mhe. Ndejembi kuwa, e-GA itaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za serikali mtandao kwa taasisi za umma na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya Serikali Mtandao.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa TEHAMA wa Wizara, Wakuu wa TEHAMA wa Idara Zinazojitegemea, Mamlaka na Wakala za Serikali, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Mikoa, Majiji na Manispaa, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Halmashauri za Wilaya na Wakuu wa TEHAMA wa Taasisi za Umma.