Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa
WANANCHI wa Kata za Mkoe wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameingia kwenye hali ya sintofahamu baada ya mimea yao ya Mahindi shambani kukauka kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu huku wakiiomba serikali kuwapatia elimu juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu .
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kupitia mikutano ya hadhara Wananchi hao wamesema kuwa mazao yao katika yaliopo shambani hasa ya Mahindi yamekauka baada ya kutumia viuatilifu na visumbufu huku ikabainika kuwa haki hiyo imetokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu hivyo.
Mmoja wa Wananchi hao Vitus Masanja amedai kuwa mazao yao mengi shambani yameungua kutokana na matumizi ya viuatilifu hivyo kiasi cha kiwango cha mavuno kuweza kupungua katika msimu huu.
Ameeleza kuwa Wakulima wa Kata hiyo wamekua wakinunua viuatilifu katika maduka mbalimbali ya pembejeo za kilimo lakini wamekuwa hawapati elimu yoyote juu ya matumizi yake na kusababisha mazao kukauka baada ya kuzitumia.
Pius Mambosasa mkazi wa kijiji cha Ilimba amesema kuwa ni ajabu kwa viuatilifu hivyo ambavyo uvitumia kuulia magugu lakini yenyewe hayafi na badala yake mazao ndiyo yanayoungua licha ya kutumia viwango vilevile vilivyoelekezwa katika karatasi ya maelekezo ya viuatilifu hivyo.
Amefafanua kuwa kinachowatia wasiwasi ni kuona kuwa Wakulima wengi wanapitia adhaa hiyo na kujiuliza kwamba ni kweli wote wanakosea maelekezo ya namna ya kuvitumia viuatilifu hivyo au kuna shida nyingine kiasi cha wao kuomba msaada kwa serikali ya kutuma Wataalamu wa kilimo wawasaidie
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Amandus Mtani kwa upande wake amewatoa shaka pamoja na kuwaagiza Maofisa Kilimo wote wa Wilaya hiyo kupita kwa wakulima na kujionea uhalisia na kuzungumza nao kupitia mikutano ya hadhara ili kuweza kuiondoa sintofahamu hiyo iliyojitokeza.
Amekiri kujionea hali hiyo shambani na kuwa wataalamu wa kilimo watapata ukweli juu ya tatizo hilo na kama tatizo itakua ni matumizi mabaya ya viuatilifu hivyo basi kazi yao itakuwa ni moja tu ya kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara na hata kwenye mashamba ya wakulima ambao wameathirika na hali hiyo.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi