May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu wa Chuo cha Mipango waaswa kutumia mafunzo waliyoyapata chuoni hapo kujiajiri

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Jenifa Omolo amewaasa wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kutumia ujuzi na mafunzo waliyoyapata kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi pekee ili kujikwamua kimaisha.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba wakati wa mahafahari ya 36 ya Chuo hicho Omolo amesema ni lazima  wahitimu hao wakatumie mbinu za ujasiriamali kama sehemu ya programu zao za mafunzo walizofundishwa kwa kuzifanyia upembuzi yakinifu, kuandaa mpango wa biashara na kuutekeleza kwa ufanisi ili kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii na kuleta mabadiliko chanya.

‘’Niwaombe wazazi, walezi, ndugu na jamaa wa wahitimu, kama mlivyoshiriki katika kugharamia masomo ya vijana hawa, msiiachie tu Serikali kuhusu hatima yao baada ya kuhitimu. Muwasaidie wahitimu watakaokuwa na mawazo ya kibiashara kupata rasilimali ya kuanzisha miradi ya kibiashara’’ amesema Omolo.

Amesema kuwa anaimani wahitimu wa chuo hicho watathibitisha vema maarifa na ujuzi walioupata Chuoni hapo kwenye ulimwengu wa kazi na  kuwakumbusha kuwa mafanikio katika ulimwengu wa leo yanahitaji moyo wa kupenda kuendelea kujifunza na ubunifu.

Amewapongeza wahitimu hao kwa kufanikiwa kuhitimu masomo yao na kuwaasa kuwa chachu ya maarifa kwa kuendelea kujifunza ili kuongeza ujuzi na ubunifu unaohitajika katika kuboresha utendaji kazini.

Aidha amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya vijana kupitia mikopo ya Halmashauri pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu kupitia Benki.

Pia Omolo amebainisha kuwa  Serikali kwa upande wake itaendelea kukiwezesha Chuo kibajeti ili kiweze kuwa na miundombinu bora na rasilimali watu inayokidhi mahitaji ya utoaji wa elimu kwa viwango bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Martha Qorro, ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga bajeti ya kugharamia uendeshaji wa chuo pamoja na kukiwezesha kutekeleza mradi wa upanuzi wa chuo hicho.

Pia aliuhakikishia umma kuwa baraza la uongozi wa chuo hicho linaendelea kuhakikisha kuwa kinatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi zaidi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo ya Vijijini Prof. Hozen Mayaya, amesema kuwa pamoja na chuo hicho kutekereza baadhi ya miradi kupitia ruzuku ya Serikali pia chuo hicho kwa mwaka 2021/22, kimetekeleza mradi wa upanuzi wa eneo la kituo cha mafunzo Kanda ya Ziwa kwa kukamilisha ulipaji fidia ya Sh. bilioni 1.73 kwa wananchi kwa kutumia mapato ya ndani.

Ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kujiajiri kuimarisha mazingira ya mikopo ya vijana kupitia bajeti za Halmashauri za wilaya pamoja na kupunguzwa kwa riba za mikopo ya benki.

Jumla ya wahitimu 6,225 wakiwemo wanawake 3503 na wanaume 2,722 wamehitimu mafunzo yao na kutunukiwa shahada za awali, stashahada na astashahada katika programu 28 kwenye mahafali ya 36 ya Chuo Kikuu cha Mipango Kampasi ya Dodoma.