April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagonjwa wa Corona nchini wafikia 24

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imethibitisha kuwepo kwa kesi mpya nne za maambukizi ya virusi vya Corona (COVID- 19) zilizopatikana Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar na kufanya kuwepo kwa jumla ya kesi 24 zilizoripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ilieleza kuwa wagonjwa hao ni pamoja na wagonjwa wawili ambao wametolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar Aprili 5, mwaka huu.

Wagonjwa wapya wawili wa Tanzania Bara ni mwanaume mwenye umri wa miaka (41) raia wa Tanzania, mfanyabiashara mkazi wa Mwanza aliyeingia nchini kutoka Dubai Machi 24, 2020 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Baada ya hapo alielekea Mwanza Machi 29, 2020 ambapo alichukuliwa vipimo na kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mgonjwa mwingine ni mwanaume mwenye umri wa miaka 35 raia wa Tanzania, mkazi wa Dar es Salaam, mfanyabiashara.

“Wagonjwa wote wako chini ya uangalizi wa watoa huduma za afya katika vituo maafum vya tiba Dar es Salaam, Zanzibar na Mwanza,” alisema Waziri Ummy.

Alisema Wizara ya Afya inaendelea kuwafuatilia watu wa karibu (contacts) waliowahi kukutana na watu hao ili kudhibiti maambukizi mapya nchini.

“Serikali inatoa msisitizo kwa wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID- 19) hususan kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imewasisitiza wananchi kuzingatia maelekezo mengine yanayohusu kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kukaa umbali usiopungua mita moja kati ya mtu na mtu.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Kassim, amewaagiza Wakuu wa mikoa nchini waimarishe ulinzi kwenye vituo vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kuwaweka watu wote wanaoingia nchini na wahakikishe hakuna anayetoka ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya Corona.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Kamati zao za Ulinzi na Usalama za Mikoa ya Mipakani ya Arusha, Rukwa, Katavi, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Mara, Pwani, Ruvuma, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Kagera, Kigoma na Songwe.

Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao waendelee kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na wahakikishe wageni wote wanaoingia nchini wanapelekwa kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kuangaliwa kama wanamaambukizi ya COVID-19.

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa wasimamie na wahakikishe watoa huduma katika maeneo hayo wakiwemo walinzi wanapatiwa vifaa kwa ajili ya kujikinga ili wafanye kazi zao bila ya kuwa na mashaka.

“Imarisheni vituo na simamieni watu wasitoke kwenda mitaani na lazima washirikiane ili maambukizi yasizidi kusambaa nchini. Fuatilieni historia za watu wanaoingia nchini kuona maeneo waliyotembelea katika kipindi cha siku 14 kabla ya kuingia nchini.”Alisema.

Kwa upande wao wakuu hao wa mikoa walisema wanaendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali kuhusu namna ya kukabiliana na virusi vya Corona na kuhakikisha havisambai zaidi nchini.