January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagombea watano wateuliwa kuwania Jimbo la Ilemela

Na Judith Ferdinand,Mwanza

JUMLA ya wagombea watano kutoka vyama vya CCM,CHADEMA,ACT-Wazalendo, Demokrasia Makini na ADC wamekidhi vigezo vya kugombea ubunge Jimbo la Ilemela hivyo wameteuliwa kuwania kiti hicho.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela John Wanga , akizungumza jana wakati akitaja majina ya wagombea waliokidhi vigezo na kuteuliwa na tume ya uchaguzi kupeperusha bendera za vyama vyao katika kinyanganyiro Cha nafasi ya Ubunge Jimbo hilo.Picha zote na Judith Ferdinand

Uteuzi huo ulifanyika jana baada ya wagombea kurudisha fomu kwa msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela John Wanga.

Wanga amesema majina ya wagombea walioteuliwa ni Dkt.Angeline Mabula(CCM),Graysona Warioba(CHADEMA),Mkiwa Adam Kimwanga(ACT-Wazalendo), Shabani Haji Itutu(ADC) na Mohamed Msanya(Demokrasia Makini).

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela John Wanga , akipokea fomu za mgombea Ubunge kupitia CCM Dkt.Angeline Mabula.

Amesema,majina ya wateuliwa hao yamebandikwa katika mbao ya matangazo ofisi kuu ya halmashauri ambapo inatoa fursa kwa wenye pingamizi kuwasilisha ndani ya masaa 24 baada ya kutangazwa majina hayo.

“Jumla ya vyama 14 vilijitokeza kuchukua fomu huku 3 vilishindwa kurejesha fomu hizo 11 vikirejesha fomu ya uteuzi na mara baada ya kuzipitia fomu hizo vyama 5 pekee ndio vilikidhi vigezo na kuteuliwa kugombea katika kinyanganyiro hicho ikiwemo CCM, ACT-Wazalendo,ADC, CHADEMA na Demokrasia Makini huku DP, CUF, CCK, NRA, SAU na NCCR Mageuzi wagombea wao walienguliwa kwa kutokidhi vigezo na masharti ikiwemo kukosa wadhamini ambao kwa mujibu wa kabuni ya uchaguzi wanapaswa kuwa 25 na kutolipa dhamana ya uteuzi,”amesema Wanga.

Kwa upande wake mgombea Ubunge kupitia CCM Dkt.Angeline Mabula ambaye anatetea kiti hicho,amesema anaimani wataenda kuweka mafiga matatu na zawadi yao kwa wananchi ni uadilifu na utumishi uliokikuka huku akikishukuru chama chake kwa kurejesha jina lake na hatimaye tume kumpitisha ili akapeperushe bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wagombea waliojitokeza kurehesha fomu za kuwania Ubunge Jimbo la Ilemela kwa Msimamizi wa Uchaguzi waJjmbo hilo.