Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
MGOMBEA Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ukerewe, Joseph Mkundi amewaomba wananchi wamchague mgombea urais kupitia chama hicho Dkt. John Magufuli kwani kwa kipindi cha miaka mitano amejenga uchumi wa wananchi na amehakikisha shida za wananchi zimetatuliwa.
Miongoni mwa mambo makubwa aliyoyafanya ni kuboresha mazingira ya elimu bure kwa watoto kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, ameimarisha usafiri wa majini ikiwemo MV.Ukara ambacho kipo kwenye hatua ya mwisho.
“Pamoja na mengine naomba mumpe tena nafasi kwa miaka mitano ili aendelee kutusaidia nchi yetu kwenye uvuvi kwani amekubali nyavu ziunganishwe ili kuvua sangara hivyo kwa heshima kubwa naomba mpigie kura nyingi za ndio ili akatuletee maendeleo na mtuchague Wabunge wake na Madiwani tunaotokana na CCM ili tukamsaidie katika kuwaletea maendeleo,” amesema Mkundi.
Mgombea katika jimbo la Sumve, Kasalali Mageni, amesema uchaguzi huu ni kati ya wananchi wanaonufaika na umeme na wale wanaopinga wasipate umeme,ambapo wakati Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa vinapata umeme ni asilimia 16.4 lakini mpaka sasa ni asilimia 66.7 vinafaidika na umeme.
Kupitia Magufuli, elimu bure imetolewa kuanzia chekechea hadi kidato cha nne ambapo imetoa fursa kwa watoto wa wanyonge kwenda shule na kupata elimu na inaonyesha ufaulu umeongeza toka mwaka 2015 ilikua asilimia 67 wakati anaingia madarakani hadi sasa ni asilimia 87 pia wanafunzi waliokuwa wanamaliza elimu ya msingi na kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa shule za Serikali umeongezeka.
Mgombea wa Jimbo la Kwimba, Sharifa Mansoor amesema kupitia Dkt.Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano katika jimbo lake changamoto ya maji imeweza kutatuliwa kwa kiwango kikubwa kwani kata takribani 14 zimepata umeme, shule na mabweni yamejengwa, fedha zimetolewa kwa ajili ya hospitali ya Wilaya na chuo pia nchi imebadilika hakuna umeme wa mgao kama huko nyuma.
Eric Shigongo, anayejombea kupitia jimbo la Buchosa amesema, wananchi wachague vitendo na siyo maneno kwani wote ni shamahidi Tanzania imebadilika sana kutokana na uongozi wake imara .
Kwa upande wake Stanslaus Mabula anayegombea ubunge katika Jimbo la Nyamagana amesema, jimbo hilo katika kipindi cha miaka 5 wana miradi isiyopungua 400 na kwa miaka 38 Nyamagana ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya maji lakini zaidi ya bilioni 66 zimekwenda kutatua changamoto ya maji ambapo maeneo yote ikiwemo ya milimani yatapata maji.
Asilimia 102 ya wanafunzi wananufaika ambapo kwa kipindi hicho madawati 31,000 na madarasa zaidi ya 400 yamejengwa pia barabara za mjini na pembezoni zaidi ya km 9zilikuwa za vumbi lakini sasa zaidi ya km 9 zimejengwa kwa kiwango cha lami pia amejenga daraja la Fumagila ambalo alitoa fedha zaidi ya milioni 500 hivyo wananchi mnasababu ya kumchagua ili kuendelea kutuletea maendeleo.
“Tuhakikishe Oktoba 28 Rais,Wabunge na Madiwani wa CCM tunashinda kwa kura za kishindo ili kuleta maendeleo na tunapo jumuisha haya mafanikio ni kutokana na Rais kutupa watendaji wazuri ambao wamesimamia miradi kwa kushirikiana na viongozi wa dini tukiongozwa na yeye ambaye ni mtendaji Mkuu katika taifa,” amesema.
Naye mgombea Ubunge kupitia CCM Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula amesema, anamshukuru Rais kwa kumuamini baada ya wanaIlemela kumuamini hivyo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amesaidia kupunguza migogoro mingi ya ardhi ambapo pia ameisha toa takribani bilioni 4 kwa TANAPA kwa ajili ya kupima na kupanga matumizi sahihi ya ardhi ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji pia kutokana na wananchi wengi kuvamia maeneo aliona bora kuwa rasimishia ili waendelee kufanya shughuli za maendeleo.
“Nikushukuru wewe kwa kuendelea kutuletea miradi ya kimkakati mingi ya maendeleo ,zaidi ya vijiji 650 vilikuwa vimevamia hifadhi za taifa na ulilidhia kwa moyo mkunjufu waweze kupimiwa na kupangiwa matumidhi sahihi ya ardhi ili wakulima na wafugaji waweze kuishi kwa amani bila migogoro,”amesema Dkt.Angeline.
Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kheri James amewaambia vijana wa jiji hilo kumpigia kura mgombea Urais kupitia CCM Dkt. John Magufuli ili aweze kushinda katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kwani kwa kipindi cha miaka mitano amewapa heshima vijana kwa vile ndiye Rais aliyewaletea heshima vijana na kutetea afya na elimu.
“Vijana wa Mwanza bandari iliyokuwa imesimama kufanya kazi sasa inaenda kufanya kazi na uwanja wa ndege unaenda kutoa fursa ya ajira kwa vijana Ilani ya CCM inaelekeza kuwapa mikopo vijana baada ya kuhitimu,hivyo tumpeni kura kwa wingi,” amesema James.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba