May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watakiwa kuunga mkono serikali kuhuisha michezo

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge amewataka wadau mbalimbali wa michezo kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhuisha michezo nchini ili kuwawezesha vijana kimchezo na hivyo kutengeneza timu ambayo inawezq kwenda kushindana kimataifa.

Mnyonge alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi kombe la Betika Sodo 4 Climate lenye lengo la kutunza mazingira ya ufukwe.

“Rais Dkt. Samia amekua akihamasisha michezo lakini kupitia utalii wa ndani na sasahivi mmeona kwenye soka kila goli moja ni milioni 5, hiyo imejenga hamasa kubwa.”

“Rais Dkt. Samia hayupo pekeake wamejitokeza na wadau wengine kama BETIKA ambapo mshindi anaondoka na kitita kikubwa”.

Kuhusu utunzaji mazingira, Mnyonge alisema wao kama halmashauri ya kinondoni wamejitahidi beach ya coco na nyinginezo zinakua safi kwani ni moja ya vivutio vya utalii wa ndani

Hivyo aliitaka jamii kuzitunza fukwe hizo vizuri ili ziweze kuleta manufaa nchini.

“Tumeona umuhimu wa kutunza fukwe hizi leo mchezo wa mpira wa soka la ufukweni hapa,mpira umechezwa hapa yote haya ni manufaa ya kutunza fukwe zetu”Alisema Mnyonge.

Kadhalika, Mnyonge aliishukuru BETIKA kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kauli mbiu isemayo “Shabikia Soka na siyo uharibifu wa Mazingira”.

Naye Meneja wa Betika, Samwel Lawarence, alisema Sodo ni ligi ambayo imeleta Hamsha kuelekea mtoko wa kibingwa awamu ya 5 ambapo wanawake na wanaume wameshiriki.

“Tangu tumeanza kampeni ya mtoko wa kibingwa tumefanikiwa kuleta jumla washindi 400 kwa ndege kutoka mikoa yote nchini ambapo Msimu wa 4 washindi wa mtoko wa kibingwa walikuwa 50 saivi wameongezeka mpaka 100″Alisema Lawarence.