December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waombwa kujitokeza kusaidia waathirika wa mafuriko

Na Martha Fatael, TimesMajira Online,Moshi

WAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi waishio ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na jamii kwa ujumla wameomba kuendelea kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko zaidi ya 70 waliohifadhiwa shule ya sekondari Lucy Lameck mjini hapa.

Waathirika hao wanahitaji magodoro, mashuka, nguo za aina mbalimbali za kiume na kike,vyakula na bidhaa nyingine za kibinadamu kwani baadhi yao hawakufanikiwa kuokoa vitu wakati walipokumbwa na mafuriko.

Diwani wa Viti maalum Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Faidha Hemed amesema hayo wakati alipowatembelea waathirika wa mafuriko katika shule ya sekondari Lucy Lameck iliyopo Kata ya Majengo mjini hapa.

“Nitoe rai kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kuja kutoa msaada kwa waathirika hawa,tutoe tulichonacho kwani hii ni ajali,hata hivyo niishukuru serikali kwa jitihada zinazoendelea hadi sasa,” amesema.

Usiku wa kuamkia Aprili 25 mvua kubwa ilinyesha katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Moshi na kusababisha vifo vya watu saba huku ikibomoa baadhi ya nyumba, kuharibu mali na miundombinu mingine.

Awali Ofisa Ustawi wa Jamii na Msimamizi wa Kambi ya Waathirika wa mafuriko Kata za Msaranga na Mji Mpya, Kiweray Macha amesema hali ya kambi ni nzuri na waathirika wanahudumiwa vyema ambayo ina watu zaidi ya 70 na wanahitaji misaada ya kibinadamu kama chakula na mavazi ili kuwasitiri.

Aprili 25 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema baada ya mafuriko kamati ya maafa inaendelea na tathmini kujua athari zilizopatikana huku waathirika wakiendelea kuokolewa.