November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa Misitu waipa neno TCB

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Mafinga

WADAU wa sekta ya misitu wameipongeza Benki ya Biashara (TCB) kwa kuunga mkono jitihada za kuinua sekta hiyo, lakini wameitaka benki hiyo kuboresha mwonekano wa ofisi za tawi lake mjini hapa na kwingineko nchini.

Wakizungumza nyakati tofauti katika mahojiano, wateja wameitaka benki hiyo kuinua hadhi ya ofisi zake ili zilingane na hadhi ya huduma zake.

“Ombi langu mimi kwa uongozi wa TCB ni kulikarabati jengo la tawi la Mafinga ili liwe na mwonekano mzuri kwa wateja wake hali itakayosaidia kuwavuta wateja wengi zaidi,” amesema Simon Mbilinyi

Mbilinyi, ambaye ni mzalishaji na msambazaji wa mbao Wilayani Mufindi na nje ya wilaya, alisema TCB ina huduma rafiki kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla, hivyo ikiboresha miundombinu ya tawi lake itazidi kuongeza wateja, kwani mwonekano pia ni sehemu ya kujivutia biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya mikopo ya mashine za kuchana mbao, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Servi Ndumbaro naye aliishauri TCB kuyafanyia kazi maombi na maoni ya wadau wake kwani hali ya jengo hilo halilingani na hadhi ya benki ilipo sasa kimtaji.

“Kuwezesha mikopo ya mashine za kuchana mbao kwa wafanyabiashara inaonesha ni jinsi gani benki ilivyo kimtaji. Hivyo ni vizuri benki ikaboresha jengo la tawi lake ili liweze kuendana mazingira ya sasa kiushindani,” amesema Ndumbaro

Mwonekano wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Tawi la Mafinga ambalo limekuwa likilalamikiwa na wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutokana na uchakavu wa jengo hilo kuwa tofauti na hadhi ya benki hiyo kibiashara. Na mpiga picha wetu.

Ameeleza kuwa ushindani wa biashara unategemea huduma zinazotolewa na benki pamoja na mwonekano wa mahali inapotolewa huduma yenyewe. Hivyo kuna haja ya kuboresha jengo lake la tawi la Mufindi ili liwe la kisasa na kuvutia kibiashara.

Chesco Njawike mfanyabiashara wa mbao Halmashauri ya Mji Mafinga, ameahidi kuwa balozi wa huduma za TCB kwa wafanyabiashara wenzake wafungue akaunti katika benki hiyo ili wanufaike na uwepo wake katika wilaya yao.

Joseph Kalindo amesema ofisi za TCB lazima ziwe na mvuto. “Ukiangalia kwa undani utagundua kwamba pengine hii ndiyo benki kongwe kuliko zote nchini. Lakini ofisi zake hazina mvuto. Hali hii inalisaliti benki hii na dira yake,” amedai Kalindo.

Dorothy Lweru amesema ofisi za tawi hazivutii, ingawa amekiri kuwa hana akaunti katika benki hiyo. “Hadhi ya ofisi hizi ni tete, iboreshwe. Mimi sina akaunti lakini nitaifungua hivi karibuni ili niwe na sifa ya kuomba mkopo,” ameeleza.

Meneja wa TCB Tawi la Mafinga, Priscillah Mollel amesema wateja wengi wanafurahia huduma wanazozitoa ikiwemo mikopo kwa wastaafu, mikopo ya vikundi yenye riba nafuu na huduma iliyozinduliwa hivi karibuni ya mikopo ya mashine.

“Malalamiko ya wateja wengi yapo kwenye miundombinu ya ofisi haipo rafiki katika kuvutia wateja kufanya huduma za kibenki na TCB, nashukuru kwa viongozi wa Serikali na wadau kulisema hili natumaini litafanyiwa kazi,” amesema Mollel

Hivi karibuni TCB, Taasisi ya kuendeleza Misitu nchini (FDT) na Kampuni ya kusambaza mashine ya Lonagro Tanzania wamekubaliana kujenga utaratibu wa kutoa mikopo ya rabi nafuu kwa wajasiriamali ili wapate mashine za kuchana mbao na kuboresha uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.