May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wa madini kunufaika na ofisi ya madini Geita

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa, wachimbaji wa madini watanufaika na ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Madini Geita katika elimu kuhusu Sekta ya Madini, utoaji wa leseni za uchimbaji, biashara pamoja na leseni za uchenjuaji madini ili wachimbe kwa tija.

Hayo yameelezwa Oktoba 28, 2021 na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Issa Nchasi wakati wa kikao cha makabidhiano ya eneo la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Madini Geita kwa Mjenzi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Inter Consult Ltd katika tukio lililofanyika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita.

Ameeleza kuwa, Wizara ya Madini imekabidhi eneo la ujenzi wa ofisi pamoja na michoro kwa Chuo Kikuu cha MUST ili waanze ujenzi rasmi.

Pia, amesema wizara inajenga jengo la Ofisi ya madini Geita ili litumike kwa shughuli za madini na kusisitiza kuwa, jengo litatumiwa na ofisi ya madini ya Geita pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini Geita.

Aidha, Nchasi amewataka wafanye kazi muda wote ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo ndani ya muda uliopangwa. Amesema ni mategemeo ya Wizara ya Madini kuwa watafanya kazi vizuri na kukamilika ndani ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 kwa sababu Fedha zimetolewa mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Naye Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Inter Consult Ltd, Arch. Beno Matata amesema, makabidhiano ya eneo la ujenzi yamekamilika kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa jengo la ofisi ya madini Geita ambapo amekabidhi kwa mkandarasi ramani ya jengo hilo ili utekelezaji uanze. Amesema mkandarasi tayari amekabidhiwa eneo la ujenzi kilichobaki ni kazi tu kukamilisha mapema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Chuo Kikuu cha MUST, Mhandisi Ivor Ndimbo ameshukuru Wizara ya Madini kwa kupewa kandarasi ya ujenzi wa ofisi hiyo na ameaidi kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Mhandisi Ndimbo ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuleta mradi huo Geita ambapo amesema ni mradi mkubwa kwa mkoa na amewahakikishia viongozi wa wizara kuwa, mradi utatoa fursa ya ajira kwa wakazi wa Geita ili wanufaike nao na kusisitiza mradi utakamilika katika kipindi kilichopangwa na wizara.

Kikao cha utiaji wa saini na makabidhiano ya ujenzi wa jengo la madini Geita kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara na Tume ya Madini ambapo ujenzi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 4.2 utaanza rasmi na kukamilika katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Eneo lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Madini ya Geita