May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachambuzi wa TEHAMA watakiwa kuongeza elimu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WACHAMBUZI wa mifumo ya TEHAMA (Business Analysts) katika taasisi za umma, wametakiwa kuongeza elimu na kupata maarifa mapya mara kwa mara, ili kuweza kuendana na kasi ya ukuaji wa mabadiliko ya teknolojia mpya zinazoibuka, ikiwemo ujuzi katika uchambuzi wa takwimu pamoja na akili bandia.

Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Ushauri na Uelekezi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),Joan Valentine, wakati akifungua mafunzo ya siku sita kwa Wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA yanayofanyika katika ofisi za Kambarage Tower jijini Dodoma.

Aidha,Joan aliwataka Maafisa hao kujifunza stadi mbalimbali ikiwemo teknolojia ya akili bandia na uchambuzi wa takwimu, ili ziwasaidie kupambana na mabadiliko ya teknolojia yanayoibuka duniani mara kwa mara na kuhakikisha teknolojia hizo zinasaidia ukuaji wa taasisi zao.

“Kwa sasa dunia inazungumza kuhusu akili bandia, hivyo wachambuzi wa mifumo lazima muwe na ujuzi wa hizi teknolojia ili kuzisaidia taasisi zenu katika utendaji kazi wa kila siku”,amesema Joan.

Vilevile,amewataka maafisa hao kuona umuhimu wa kujifunza stadi tepe ‘soft skills’ ili ziweze kuwasaidia katika kupambana na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ulimwengu kote.

“Kwa sasa TEHAMA inatoka kuwa fani saidizi ‘supporting tool’ hadi kuwa fani wezeshi ‘enabling tool’ hivyo, mnatakiwa muwe wajuzi zaidi katika sekta ya TEHAMA ili kuzisaidia taasisi zenu katika kupiga hatua katika utendaji kazi wa kila siku”, amesisitiza.

Mratibu wa Mafunzo hayo Ceaser Mwambani ambaye pia ni Mchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA e-GA, alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa hao, katika maeneo ya Uchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA, Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, Miongozo, Viwango, Usimamizi, Ubora na Usalama wa Mifumo ya TEHAMA Serikalini.

“Kupitia mafunzo haya, tunaimani kuwa, washiriki wote hapa watakuwa na uelewa zaidi kuhusu uchambuzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA Pamoja na kuweza kutoa mchango mzuri kwenye taasisi zao ili kuwa na miradi yenye tija kwa taifa”, amefafanua.

Mafunzo hayo yanayotarajiwa kukamilika Novemba 25, mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za e-GA za kuhakikisha inashirikiana na kuzijengea uwezo taasisi za umma katika kukuza Serikali Mtandao