May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WABUNGE waridhishwa,ubora kituo jumuishi cha utoaji haki mkoa wa mwanza

Na Daud Magesa,TimesMajira Online,Mwanza

KAMATI ya Bunge ya Utawala Bora,Katiba na Sheria, imevutiwa na mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoa wa Mwanza na kupongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa na nzuri ya kuboresha eneo la utoaji haki na kuwezesha wananchi kuhudumiwa karibu.

Imesema mradi huo kuwa unaakisi mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili madarakani.

Wakichangia taarifa ya mradi huo uliogharimu bilioni 8.56 baada ya kuutembea wabunge hao waliridhishwa nao na kuipongeza serikali kwa juhudi kubwa inazofanya za kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwapunguzia adha ya kuzifuata umbali mrefu.Wamesema yapo mengi ya maendeleo na mafanikio yamefanywa na serikali kama jengo la kituo jumuishi cha utoaji haki na mengine ambapo walishauri Rais Dk.Samia asemwe kwa vitendo watu wafahamu wasiseme hakuna kilichofanyika.

“Mradi huu umetekelezwa kwa weledi,pongezi za dhati ziende kwa Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na serikali yake,”amesema Salum Mohamed Shafi,Mbunge wa Chonga (ACT-Wazalendo).

Mbunge wa Mlalo,Abdallah Shangazi amesema kazi imefanyika kwa weledi, ni kitu kikubwa na jambo kubwa ndani ya nchi, utu na ubinadamu umezingatiwa katika mradi huo wa kituo cha utoaji haki,hivyo maono hayo yaendelee kuenziwa na huduma za namna hiyo zifike mikoa yote nchini.

“Jambo kubwa limefanyika hapa kwenye eneo la utoaji haki ingawa mfungwa hachagui gereza ipo siku baadhi wanaweza kuomba kesi zao zisikilizwe hapa,inaonekana huduma kwenye mahakama ni nzuri, naomba bajeti ya ukarabati itengwe kila mwaka ili majengo haya yadumu muda mrefu,”amesema Shangazi.

Aidha Mbunge wa Viti Maalum (Wafanyakazi),Dk. Alice Kaijage,amesema kazi nzuri ya kuboresha mhimili wa mahakama imefanyika na kituo hicho jumuishi cha utoaji haki kimezingatia vitengo mbalimbali kikiwemo chumba cha akinamama cha kunyonyeshea watoto na kuomba ramani ya jengo hilo iwe endelevu kwa mikoa mingine.

Mbunge wa Nyangh’wale, Hussein Nassor Amar,amesema biashara ni matangazo na kushauri huduma zinazotolewa kwenye kituo hicho jumuishi cha utoaji haki zifahamike kwa wananchi wapate fursa ya kuzitumia.

Kwa upande wake Mbunge wa Singida Kaskazini,Ramadhan Ighondo aliipongeza serikali kwa maboresho hayo na kwa vile rasilimali za kutosha kuwahudumia Watanzania zipo tunawajibika kuvitunza vituo jumuishi vya utoaji haki vitutuhudumie kwa muda mrefu.

Amesema jamii ihakikishe ina yathamini na kuyatunza majengo hayo na kumshukuru Rais kuridhia kuleta fedha zilizoidhinishwa na bunge na kuviomba vyombo vya habari kupeleka taarifa sahihi wananchi watumie huduma za vituo jumuishi vya utoaji haki .

Naye Waziri wa Katiba na Sheria,Dk.Damas Ndumbaro,amewashukuru wabunge kwa kuridhika na utendaji wa serikali pia matumizi ya bajeti iliyotengwa na kumpongeza Rais Samia kwa namna anavyoiongoza nchi na serikali hususani Wizara ya Katiba na Sheria.

Ameeleza kuwa wizara hiyo ina bahati ambapo imepewa upendeleo wa kuhudhuria matukio matano huku mkuu huyo wa nchi akiwa mgeni rasmi na akimshukuru anavyopigania bajeti ya mhimili wa mahakama, zamani hali ilikuwa mbaya.

“Mabadiliko ya mahakama ni ya kasi ambapo majengo 9 yako kwenye mkakati wa kujengwa kwa kiwango na ubora ili kuleta huduma ya sheria na haki karibu na jamii,pia mabadiliko makubwa hayo ya miundombinu ya mahakama, yamewarahisishia majaji na mahakimu kusikilizana kutoa hukumu kwa muda mfupi,”amesema Dk.Ndumbaro.

Aliongeza kuwa mahabusu na wafungwa wanaweza kusikiliza kesi zao wakiwa gerezani bila kufika mahakamani baada ya kuwekwa vifaa vya TEHAMA kupitia maboresho hayo yanayofanywa na serikali ya CCM.

Awali Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu, Leonard Magacha, amesema mradi huo wa jengo la ghorofa tatu uliogharimu sh.bilioni 8.561 utawezesha wananchi kufikia huduma za mahakama kwa urahisi na karibu.

Pia huduma katika jengo moja kutarahisisha utendaji,kupunguza nakisi ya rasilimali watu na kutumia idadi ndogo ya watumishi, matumizi ya rasilimali chache za umeme,maji, ulinzi na usafi na hivyo wananchi watumie fursa zilizopo kwenye jengo hilo ili kurahisisha utoaji haki kwa wakati.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa Mahakama Kuu,Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza,ni miongoni mwa majengo sita yaliyozinduliwa na Rais Samia, Oktoba 6, 2021 yakilenga kuboresha huduma za utoaji haki na kuzisogeza karibu na wananchi.