May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waasi wakamatwa Kaskazini mwa Chad

N’DJAMENA, Mkuu wa utawala wa Jeshi la Chad, Abakar Abdelkerim Daoud amewaambia waandishi wa habari kuwa, waasi walioanzisha mashambulio katika jimbo la Kanem Kaskazini nchini Chad wametekwa na jeshi pamoja na silaha na vifaa vyao.

Daoud amesema hali imerudi kuwa ya kawaida tena. “Na ninataka kuwahakikishia wananchi kwamba hawana haja ya kuwa na wasiwasi, mambo yamemalizika,”amesema.

Aidha, hii ni mara ya pili kwa jeshi la Chad kutangaza ushindi katika vita hivyo vilivyoanza mapema mwezi Aprili yaliosababisha kifo cha Rais wa muda mrefu Idriss Deby kwenye uwanja wa mapambano mwezi uliopita na baadae kuanza tena.

Kundi la waasi la kutaka kuleta mageuzi nchini Chad (FACT) halikujibu ombi la waandishi habari kutoa maoni yao.
Hata hivyo mamia ya wapiganaji waliokamatwa na jeshi waliwekwa kwenye uwanja wa kambi kuu ya kijeshi mjini N’djamena ili waandishi wa habari kushuhudia ushindi wao.

Mkuu wa masuala ya kijeshi wa waasi wa kundi la FACT, Mahadi Bechir akiwa miongoni mwa waliokamatwa, ametoa wito kwa waasi wenzake ambao hawajakamatwa bado kujisalimisha na kujiunga na mfumo wa kisheria nchini humo ili kwa pamoja waweze kuchangia katika ujenzi wa taifa.