May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muonekano wa mji wa Mogadishu ukiwa katika hali ya utulivu hivi karibuni. (Picha na REUTERS/Feisal Omar).

Polisi wauawa,ghasia zaendelea Jerusalem

MOGADISHU, Mshambuliaji wa kujitoa mhanga amewaua maafisa watano wa polisi mjini Mogadishu, Somalia kwa bomu.

Mlipuko huo umesababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliyevalia vazi la kujilipua ambaye aliwafuata maafisa hao nje ya kituo cha wilaya ya Waberi juzi majira ya usiku.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, maafisa watano wa polisi ni miongoni mwa watu wasiopungua sita waliouawa Jumapili iliyopita jioni na bomu la kujitoa mhanga mjini Mogadishu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi la Somalia,Meja Sadiq Aden Ali amesema kuwa, makamanda wawili wa polisi ni miongoni mwa waliouawa.

Aidha, Meja Ahmed Abdullahi Bashane ambaye ni Kamanda wa Wilaya ya Waberi huko Mogadishu na Meja Abdibasid Mohamud Agey ambaye ni Naibu Kamanda wa zamani wa idara ya polisi ya Weliyow Adde, waliuawa pamoja na maafisa wengine watatu wa polisi.

Raia mmoja ambaye alikuwa akiishi karibu na kituo hicho cha polisi pia aliuawa katika mlipuko huo.Watu sita wengine walijeruhiwa katika mlipuko huo, kulingana na taarifa ya polisi.

Shahidi ambaye hakuweza kutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama alisema, Bashane alikufa katika eneo la tukio wakati Agey alifariki kutokana na majeraha aliyopata baada ya kuondolewa kwenda sehemu nyingine kwa matibabu.

Saa tatu kabla ya mlipuko huo, Bashane alituma ujumbe wa “Mother’s Day” akimtakia heri mama yake kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Jerusalem

Mbali na hayo, maafisa wa Palestina na Israel wamelaani kuongezeka kwa ghasia kwenye uwanja wa msikiti mtakatifu wa al-Aqsa na kwenye mitaa ya Jerusalem Mashariki, huku kila upande ukimlaumu mwingine kwa kusababisha ghasia hizo.

Pia Wapalestina na Waisraeli wameandamana kuadhimisha siku ya Jerusalem au siku ya al-Quds wakati mji huo ulipotekwa na kukaliwa na Israel wakati wa vita vya siku sita vya 1967.

Wakati hayo yakiendelea watu 300 waliripotiwa wamejeruhiwa kutokana na mapambano kati ya polisi na waandamanaji kwenye uwanja wa Mskiti wa al-Aqsa ambao ni eneo la tatu takatifu kwa Waislamu na la kwanza takatifu kwa Wayahudi.

Kwa karibu mwezi mmoja katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, Wapalestiina wamekuwa wakipambana wakati wa usiku na polisi wa Israel kwenye uwanja wa al-Aqsa kulalamika dhidi ya hatua kali zilizowekwa na polisi kuingia msikitini humo kutokana na juhudi za kupambana na COVID-19.

Ghasia zimezidi siku za hivi karibuni na maafisa wa afya na chama cha Hilali Nyekundu cha Palestina walisema karibu watu 500 walijeruhiwa wiki iliyopita wengi wakiwa na majeraha ya risasi za mpira.

Aidha, ghasia hizo zinasemekana ndiyo mbaya zaidi tangu mwaka 2017 huko Jerusalem zilizochochewa na ugomvi wa muda mrefu kutokana na juhudi za walowezi wa Kiyahudi kutaka kuwaondowa Wapalestina waliokuwa wanaishi katika mji wa kale wa Jerusalem tangu mwaka 1956.

Mahakama ya chini ya mji huo ilikubaliana mapema mwaka 2021 na madai ya walowezi kuchukua nyumba za familia 29 katika mtaa wa Sheik Jarr. Lakini Mahakama Kuu iliyokuwa isikilize rufaa dhidi ya kesi hiyo wiki hii iliahirisha kikao kufuata ombi la wizara ya sheria kwa hofu ya kuzuka ghasia zaidi.

Hata hivyo, kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisma ni lazima kwa maafisa wa Israel kujizuia na kuheshimu haki za watu kukusanyika kwa amani.

Mataifa ya kiarabu pamoja na yale sita yaliyoanzisha uhusiano na Israel, yalilaani utumiaji nguvu unaofanywa na Israel. Marekani pia ilieleza wasiwasi wake kutokana na ghasia hizo.