November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari washauriwa kuutangaza utalii nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma.

WAANDISHI wa Habari nchini wameshauriwa kuiga mfano wa baadhi ya waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma walioamua kuunga mkono Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuutangaza utalii kwa kutembelea Mbuga za wanyama wao wenyewe kwanza.

Ushauri huo umetolewa jijini hapa,Machi 13,2023 na Kamshna Msaidizi Mwandamizi,Jeshi la uhifadhi Ofisi ya Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) Dodoma,Dkt.Noelia Myonga wakati akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo vya habari mbalimbali  Mkoa wa Dodoma,waliojitolea kujikita katika kuandika habari za Utalii na Uhifadhi kwa kutembelea mbuga za wanyama kwa namna tofauti tofauti.

“Nawapongeza Sana nyinyi waandishi wa Dodoma  kwakuamua kwa hiari yenu kujikita katika kuandika habari hizi kwa namna tofauti kama mlivyowasilisha katika ofisi yetu ya Tanapa natamani kuona na waandishi wa mikoa mingine wakiiga mfano wenu,

“Nakumbuka andiko lenu linasema mtakwenda kutalii katika hifadhi za Taifa Tanzania kwa kuanza na hifadhi ya Tarangire lakini mmesema mtaenda na watoto wenye mahitaji maalumu yani wasiosikia hii ni nzuri sana na haijawahi kutokea nawapongeza sana endeleeni kuwahamasisha waandishi wenzenu wa Mikoa mingine kutembelea Ofisi za Tanapa zilizopo kwenye mikoa yao kuangalia namna ya kuhamasisha utalii kwa kutumia kalamu zenu,”amesema Dkt.Myonga.

Vilevile Dkt.Myonga amesema kuwa kumekuwa na changamoto yakutokuwa na taarifa sahihi kuhusu uwezo wa kwenda kutalii kuwa gharama ni kubwa kitu ambacho siyo kweli.

Hivyo amewataka wananchi wafuatilie taarifa sahihi kuhusu gharama za viingilio ambazo amezitaja ni za chini sana ukilinganisha na kipato cha mtanzania wa kawaida.

“Watanzania wenzangu gharama za viingilio ni ndogo kwani gharama kwa mtanzania mtu mzima ni Shilingi 11,800 pamoja na VAT huku ya mtoto ni shilingi 2400 pamoja na VAT,”amesema.

Pamoja na hayo Dkt.Myonga aliwataka watanzania kujijengea utamaduni wa kutembelea hifadhi kwani watajifunza mengi kutokana na rasilimali zilizopo katika nchi yetu.

“Tanzania tuna Hifadhi 22 karibu mikoa yote kazi kubwa ya Tanapa ni kuhifadhi rasilimali zote zilizopo ndani ya hifadhi za Tanzania hivyo kunavivutio tofauti tofauti vya kutalii na kujifunza mengi kuhusu Tanzania yetu,”amesema.