March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari wapigwa msasa juu ya chanjo ya corona

Penina Malundo na Martha Fatael,timesmajira,Online


WAANDISHI wa habari nchiniĀ  wameomba kupatiwa mafunzo zaidi kuhusu ugonjwa na chanjo ya Corona kwani umeingiliwa na Imani nyingi potofu na taarifa zisizokuwa sahihi.


Kadhalika wameiomba serikali kusaidia kutoa elimu ya kutosha kwa wataalamu wa afya na kuonya kuacha kupotosha kuhusu Corona kwani baadhi wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali zinazodhoofisha jitihada za serikali katika kudhibiti ugonjwa huo.


Wakitoa maoni hayo wakati wa kikao Cha waandishi wa habari, wataalamu wa afya kilichoratibiwa na shirika la Internews kuhusu kinachoendelea kwenye ugonjwa wa Corona na chanjo zake,baadhi ya waandishi waliomba mafunzo hayo yawe endelevu.

Nakajumo James,mmoja wa wanufaikaji wa mafnzo hayo ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili kuweza kusaidia jamii kupata uelewa sahihi juu ya chanjo.


Amesema ujio wa ugonjwa wa Corona umekuwa na athari kubwa kiuchumi, kijamii na katika kila nyanja hivyo ni vyema ufuatiliaji na mafunzo ya mara kwa mara yakafanyika kwa waandishi wa habari ili waendelee kuielimisha jamii kupitia vyombo vyao.


“Tunashukuru kwa jitihada zinazofanywa na shirika hili la Internews, tunawaomba wasichoke kutoa elimu mfululizo maana Imani potofu dhidi ya ugonjwa wa Corona zinaibuka kila mara lakini pia bado tafiti zinaendelea” Amesema


Akitoa mafunzo hayo Mtaalamu wa Masuala ya Afya,Dk. Mwidimi Ndosi amewataka waandishi wa habari kuwa makini na wataalamu wanahowahoji kuhusu ugonjwa huo kwani sio wote wanaweza kueleza vyema kuhusu kirusi Cha Corona.


“Kirusi Cha Corona bado ni kipya kinabadilika badilika na tafiti bado zinaendelea kuhusu ugonjwa na chanjo hiI hivyo ni vyema waandishi wa habari wakataza kwa umakini chanzo Cha habari yake kama ni sahihi ili kuepusha mkanganyiko kwa jamii” amesema


Hata hivyo Shaban Maganga aliwataka waandishi wa habari kuandika habari nyingi zaidi zenye kusaidia kutoa elimu sahihi kwa jamii na kusaidia kudhibiti ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi.