January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vituo vya huduma za afya kuwa na mashine za kisasa za upimaji,MSD yajipanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wezee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, akipa maelezo kutoka kwa Ofisa Mdhibiti Ubora wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Kitukulu, kuhusu mashine ya kupima kemia ya mwili katika maabala ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dar es Salaam,. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu Meja wa MSD Meja Jenerali Gabriel Mhidze.

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima amesema hadi kufikia Januari mwakani vituo vya kutolea huduma za  afya,  vyote nchini vitakuwa na mashine za kisasa za upimaji katika maabara na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
 
Dkt.Gwajima, amesema hayo leo Dar es Salaam, wakati wa  ukaguzi wa mashine hizo zilizotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Mwananyamala ambapo pamoja na mambo mengine alisema hatua hiyo ni muendelezo wa mikakati inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma za afya nchini.
 
Amesema matarajio hadi ifikapo Desemba mwaka huu usambazaji wa mashine hizo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini utakuwa umekamilika na ifikapo Januari kila kituo kitaanza kuzitumia, Serikali itatoa tamko rasmi mara usambazaji wake utakapokuwa umekamilika.
 
“Upatikanaji na usambazaji wa mashine hizo umetokana na uwepo wa makubaliano mapya baina ya MSD na wazabuni ambayo yamewezesha mashine hizo kupatikana kwa gharama nafuu tofauti na hapo awali baada ya kuwaondoa madalali ambao hapo awali walichangia kuuzwa kwa bei ya juu,”amesema.
 
Amesitiza lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya afya huku akisisitiza kuwa ujio wa mswaada wa bima ya Afya kwa wote utakaowasilishwa Bungeni Novemba mwaka huu kwa ajili ya kujadiliwa utatoa uhakika wa huduma kwa kila mwananchi. 
 
“Kupatikana kwa mashine za kutosha katika vituo vyote pia kutawezesha gharama za huduma kushuka lakini pia kutaondoa ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kupata huduma  ambazo hapo awali vilikosekana katika maeneo yao kutokana na ukosefu wa mashine hizo” ameongeza Dk Gwajima
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu  wa MSD Meja Jenerali Gabriel Mhidze amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mashine hizo zinasambazwa katika vituo vyote nchini kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa ili kurahisisha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi.
 
Amesema wao kama MSD watashirikiana kikamilifu na wafanyabiashara wanaouza mashine hizo hadi utaratibu utakapokamilika huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali kujenga hospitali nyingi nchini itatoa mrejesho chanya pale ambapo huduma zote ikiwemo ya upatikanaji wa vipimo inapatikana kwa uhakika katika maeneo yote.
 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wezee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, akisikiliza maelekezo kuhusiana na usambazaji wa mashine Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Brigedia Jenerali Gabriel Mhidze.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wezee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, akipa maelezo kutoka kwa Ofisa Mdhibiti Ubora wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Kitukulu, kuhusu mashine ya kupima kemia ya mwili katika maabala ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dar es Salaam, jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Brigedia Jenerali Gabriel Mhidze.