May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Virusi vipya vya G4 vyawakosesha usingizi wanasayansi, walaji nguruwe hatarini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Beijing

Wanasayansi nchini China wamegundua aina mpya ya virusi vya mafua vilivyopewa jina la (G4) ambavyo vina uwezekano mkubwa wa kuambukiza kutoka kwa nguruwe kwenda kwa binadamu.

Mafua hayo yanatajwa kuwa hatari kwa binadamu kutokana na kile ambacho kinadaiwa kuwa, binadamu ana kinga ndogo ambayo haina uwezo wa kustahimili.

Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya ripoti ya utafiti huo ambao umechapishwa nchini Marekani na moja ya jarida la kitabibu kutoka Taasisi ya Taifa ya Sayansi (PNAS).

“Virusi vilivyopewa jina la G4, vinatoka kwa nguruwe tangu mwaka 2016 na vinaweza kuathiri binadamu,”utafiti huo umethibitisha hilo, ikiwa ni matokeo ya utafiti wa kina uliofanyika kwa nguruwe tangu 2011 hadi 2018.

Pia wanasayansi hao wana hofu kwamba, mafua hayo yanaweza kusambaa kirahisi na kusababisha mlipuko ingawa kwa sasa yanaweza yasiwe tatizo huku wakishauri suala la tahadhari ni muhimu zaidi.

Wakati hayo yakijiri huku wanasayansi wakiendelea kuchunguza kwa kina ili kupata chanjo na tiba ya virusi vya corona (COVID-19), wataalam wa masuala ya afya katika ngazi za Kimataifa wanasisitiza kuwa, huu ni wakati wa kila mmoja kuzingatia tahadhari, kwani juhudi zinaendelea kupata suluhu.

“Siwezi kujua ukubwa wa ugonjwa huu, ni suala la subira katika kujikita kutafiti kwa kina,” anasema Robert Webster, mpelelezi wa mafua ambaye alistaafu hivi karibuni katika Hospitali ya Utafiti ya Watoto ya St.Jude.

“Je! hivi vitafanya hivyo? Mungu anajua,”anasema, na kuvifananisha virusi hivyo na mchezo wa kubahatisha kama vitabadilika na kusambaa kwa binadamu.

Kin-Chow Chang ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza amesema,virusi hivyo, havijatoa tishio kubwa hadi sasa. Lakini ameonya watu wasijisahau sana kuhusu kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya awali na hivyo vipya.

Maoni ya Chang yanaungwa mkono na Martha Nelson, mtaalam wa mabadiliko ya biolojia katika Taasisi ya Kimataifa ya Kituo cha Afya cha Fogarty cha Marekani, “Uwezo ambao tofauti hii itasababisha ugonjwa ni mdogo,”anasema mtaalam huyo ambaye amebobea katika utaalam wa kuchunguza virusi vya mafua ya nguruwe kwenda kwa binadamu nchini Marekani.

Lakini alibainisha kuwa, hakuna mtu aliyejua juu ya ugonjwa wa H1N1, ambao ulienea kutoka kwa nguruwe hadi kwa watu, hadi kesi za kwanza za wanadamu zikarekodiwa 2009.

“Mafua yanaweza kutushangaza,”Nelson anasema. “Tunahitaji kuwa macho, juu ya vitisho vingine vya magonjwa ya kuambukiza hata kama COVID-19 inaendelea kwa sababu virusi havina subira ikiwa tunakuwa na janga jingine ni changamoto,”anasema.

Hayo yanajiri ikiwa mwezi Aprili 2009, Umoja wa Mataifa ulichukua juhudi mbalimbali za kushughulikia tatizo la afya lililozuka ulimwenguni, baada ya kugunduliwa homa ya mafua ya nguruwe katika baadhi ya mataifa na namna ugonjwa huo ulivyoathiri wanadamu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) wakati huo lilibainisha kwamba, walipokea ripoti za kutoka maabara ya uchunguzi wa maradhi, zilizothibitisha kwamba jumla halisi ya watu walioambukizwa wakati huo, na homa ya mafua ya nguruwe ilikuwa ni 73, na miongoni mwa idadi hiyo wagonjwa 40 walipatikana Marekani, 26 Mexico na wagonjwa wengine sita walikumbwa na maradhi nchini Canada huku mmoja alibainika nchini Hispania.