April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi watakiwa kutoa kipaumbele mikopo ya walemavu

 Na Penina Malundo,timesmajira,Online

VIONGOZI mbalimbali nchini wakiwemo madiwani,  wametakiwa kushirikiana pamoja ili kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu linapewa kipaumbele katika kupatiwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmslashauri nchini.

Fedha hizo kutolewa kwa makundi ya wanawake asilimia 4,vijana asilimia 4 pamoja na  watu walemavu asilimia 2 kwa ajili ya kuwakopesha na kufanya shughuli zao mbalimbali za maendeleo.

Aidha maofisa ustawi wa Jamii wanatakiwa kuhakikisha wanatatua changamoto zozote zinazowakumba watu wa kundi hilo ikiwemo kuhakikisha wanapatiwa mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na diwani wa kata ya Mkundi ,Seif  Chomoka wakati wa uzinduzi wa Bonaza la watu wenye ulemavu lililofanyika mkoani Morogoro.

Amesema ni jukumu la kila mtu kusimamia ulemavu kupata haki yake. Amesema kuwa ulemavu wowote unakuja kwa mapenzi ya Mungu  na wala mtu akiwa  mlemavu hakosi uwezo.

“Nitafanya kazi nanyi bega kwa bega katika kila hatua kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao za kuishi kwa amani na upendo bila kubughudhiwa na mtu yeyote,”alisema na kuongeza;

“Kutokana na uundwaji wenu wa vikundi nawahaidi kuwapatia mitaji kupitia vikundi vyenu kwa halmashauri ya manispaa,”Alisema.  Aidha alisema kuna changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo watu wenye ulemavu ikiwemo kutengwa na jamii jambo ambalo sio zuri, kwani ulemavu unakuja kwa mapenzi ya Mungu,”amesema

Kwa upande wake,msoma risala kutoka kundi la watu wenye  ulemavu ,Violeth Kilimali amesema lengo la bonanza hilo ni kufanya mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kutambua uwepo wa fursa mbalimbali ambazo watu wenye walemavu wanaweza kujihusisha kwa lengo la kujipatia kipato halali ili kuwawezesha kujikimu kimaisha.

Kilimali amesema pamoja na hayo, wameweza kuibua vipaji vipya na kutambua uwepo wa vipaji vilivyokuwepo kama  kucheza mpira, kucheza muziki pamoja na kuimba.

“Jumuiya ya watu wenye ulemavu imefanikiwa kusajiri vikundi kwa watu wenye ulemavu ambapo hadi sasa ni vikundi 14 vyenye watu zaidi ya watano katika kila kikundi,vikundi hivyo vinatambulika kisheria na vimefanikiwa kufungua akaunti benki kwa kila kikundi,”amesema na kuongeza

“sisi kama walemavu tumeweza kupata faida nyingi kutokana na mabonanza kama haya ikiwemo kuimarishwa kwa mahusiaono yetu wenyewe kwa wenyewe  na watu mbalimbali kama wakufunzi wa mafunzo ya ujasiriamali, waimbaji mbalimbali pamoja na wachezaji wa makundi mengine,”amesema Kilimali

Naye Mkurugenzi  wa Taasisi ya See Tanzania,Nicas Mahinda amesema wao kama Taasisi wamedhamuri kugusa watu wenye walemavu lengo ikiwa ni kusaidia kundi hilo  kwani wao ni wanufaika wakubwa wa mikopo ya Halmashauri.

Alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwa kundi hilo kukosa fursa ya kupata elimu elekezi ya ujasiriamali hivyo kusababishwa kushindwa kutumia fedha hizo za Halmashauri  kwenye muongozo ambao ni Sahihi.

“Sisi tumeona kuna haja ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu  ili watakapopewa hiyo mikopo waweze kunufaika nayo kwenye tija kwa kufanya shughuli za kimaendeleo  ambazo zitasaidia wao pamoja na Familia zao.

“Ndani ya mwaka mmoja Taasisi yetu italea vikundi vya watu wenye ulemavu ambao watakuwa hawatapata mikopo ya Halmashauri watapata fursa ya kufundishwa mafunzo ya ujasiriamali kwa nadharia na vitendo katika vikundi vyao na mtu mmoja mmoja tutawasimamia kwenye miradi yao na kuwapatia elimu ya utunzanji fedha ili  fedha watakaokuwa nayo watumie kwa  ufasaha ili kupata maendeleo yao,”amesema Mahinda