Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Mbeya
VIONGOZI wa kimila wa Mkoa wa Mbeya wameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa nchini.
Viongozi hao wamepongeza benki hiyo leo wakati wa ziara maalum ya kutembelea kiwanda cha Raphael Group Ltd., katika wilaya ya Uyole.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Machifu wa Mbeya jiji na vijijini, Chifu wa kabila la Wasafwa, Rodrick Mwashinga, ameipongeza TADB kwa uwekezaji wake katika kampuni ya Raphael Group Ltd. ambayo ni moja ya kampuni inayoongoza Nyanda za Juu Kusini kwa kuzalisha, kuchakata na kuuza nafaka.
“Ninapenda kuwashukuru sana TADB kwa kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa katika mkoa huu. Hii inadhihirisha imani iliyonayo TADB kwa wawekezaji wa ndani na waliotoka katika jamii zetu wenyewe,” amesema Chifu Mwashinga.
Ameongeza kwamba; “Uwekezaji huu wa TADB unadhihirisha nia yao ya kusaidia jamii katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia shughuli ya kilimo, hivyo napenda kutoa wito kwa benki hii iendelee kupanua wigo wa utoaji wake wa mikopo kwa wakulima na wawekezaji wazawa ili kuweza kujenga viwanda kama hivi vingi zaidi kuongeza ajira, kuleta uhakika wa masoko wa mazao ya wakulima na kuchagiza maendeleo ya mkoa na uchumi wa nchi kwa ujumla wake.”
Akizungumzia uwekezaji wa TADB katika kampuni ya Raphael Group Ltd., Meneja wa Kanda wa Nyanda za Juu Kusini kutoka benki hiyo, Alphonce Mukoki, amesema benki hiyo imeiwezesha kampuni ya Raphael Group kupata mashine ya kisasa ya kuchakata tani 80 ya mpunga kwa siku, mashine ya kukausha mpunga, na mashine ya uhakiki na utengaji wa rangi ya mchele.
Pamoja na hayo, benki pia imeipatia kampuni hiyo mtaji wa uendeshaji kwa ajili ya kununua mpunga na maharage kutoka kwa wakulima wadogo zaidi ya 13,000 Mbeya na mikoa ya jirani.
Mukoki pia amesisitiza nia ya benki hiyo katika kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa katika kuchagiza mageuzi ya kilimo na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
“Malengo yetu kama benki ya maendeleo ni kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa na teknolojia ya kisasa, pamoja na mtaji wa kuinua sio tu biashara zao, bali pia kuleta manufaa kwa minyororo ya thamani husika,” amesema Mukoki.
“Uwekezaji wetu katika Raphael Group Ltd. ni mfano wa kuigwa katika kazi nzuri tunayoifanya ya kuleta mageuzi katika sekta hii muhimu sambamba na Mpango wa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano iliyozinduliwa na Serikali hivi karibuni.”
Kutokana na taarifa kutoka TADB, hadi Juni mwaka huu, benki hiyo imekwisha wekeza zaidi ya sh. bilioni 30 katika Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma na Songwe, katika minyororo ya thamani 18, ikiongozwa na zao la mpunga, kakao, mahindi na kahawa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Raphael Group Ltd, Lazaro Mwakipesile, amesema kwamba nia ya ziara ya viongozi hao wa kimila ilikuwa ni kuelimisha jamii juu ya ushirikiano katika ya TADB na kampuni hiyo, pamoja na kushuhudia moja kwa moja shughuli ya kiwanda hicho ya kuzalisha, kusindika na kuuza nafaka.
Akiwasindikiza machifu hao wa Mkoa wa Mbeya, Diwani wa Kata ya Itezi, Sambwee Shitambala, aliishukuru kampuni ya Raphael Group Ltd na TADB kwa fursa ya kwenda kujifunza kuhusu ushirikiano wao na uwekezaji walioufanya katika mnyororo wa thamani wa mpunga ambao umeleta manufaa makubwa kwa jamii ya Mbeya na Nyanda ya Juu Kusini kwa ujumla.
“Ushirikiano katika uwekezaji huu kiuhakika utatangaza Mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla kama kitovu cha kuzalisha, kuchakata na kuuza mpunga,” amesema Shitambala.
Raphael Group Ltd. ni moja ya kampuni inayoongoza Nyanda za Juu Kusini katika kuchakata na kuuza nafaka aina sita tofauti. Zao la mpunga inachukua asilimia kubwa (asilimia 50) ya biashara ya kuchakata ya kiwanda hicho, ikifuatia na maharage (asilimia 20), karanga (asilimia 10), na mahindi (asilimia 5).
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati