Na Penina Malundo,timesmajira,Online
WITO umetolewa kwa Viongozi wa dini,Serikali za mitaa pamoja na watu wa madawati ya kijinsia kuisaidia a jamii inayokabiliana na hali ya ukatili wa kijinsia husasani wanawake na watoto.
Akizungumza hayo juzi katika Mkutano uliowahusisha viongozi hao mkoani Dar es Salaam,Mwenyekiti wa Taasisi ya Women Tapo Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tabata Women Tapo,Stella Mbaga amesema lengo la mkutano huo ni kuendelea kuwasaidia wakinamama wanapopata changamoto za ukatili wa kijinsia katika nyumba zao kujua wapi wanaweza kupata msaada.
Amesema mara kwa mara shirika lao limekuwa likiwakutanisha wamama wakiwemo wale wanaofanya shuguli zao sokoni na wachuuzi na kuwaelimisha juu ya masuala mbalimbali ikiwemo suala la kutofumbia macho ukatili wa kijinsia wanaokumbana nao majumbani au masokoni kwa lengo la kuhakikisha wanaripoti sehemu sahihi.
“Shirika letu ni miongoni mwa mashirika ambayo yanajishughulisha na uelimishaji wa wakinamama wa masoko,wasichana na watoto kujua haki zao mbalimbali,”amesema na kuongeza
“Haya Matapo yapo mengi nchini ,ila sisi TAPO letu ni la Tabata imekuwa ikitoa elimu mbalimbali ikiwemo Jinsia,Afya na fedha na imekuwa msaada mkubwa kwa wamama wa Tabata na kusaidia kwa kiasi kikubwa wamama kujisimamia hata pale wanapotewkelekezwa na wanaume zao,”amesema
Aidha amesema mkutano huo umekuja kuwasaidia viongozi wa serikali za mitaa,viongozi wa dini na watu wa madawati ya kijinsia kuelewa suala zima la ukatili wa kijinsia.
Amesema viongozi hao watakapoelewa dhana nzima ya ukatili wa kijinsia itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa wamama wanapoenda kutoa taarifa za hali hiyo inapowatokea viongozi hao wajue wanawasaidiaje.
“Mkutano wa leo utakuwa chachu kubwa kuwafungua juu ya matatizo hayo ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili wa kulawiti Watoto ambao kwa sasa umekuwa ukishika kasi,”amesema
Kwa Upande wake Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjilisti la Kiluteli (KKKT)ushirika wa Tabata Shule ,REV. Richard Kibwana amesema ni vema suala la ukatili wa kijinsia kuendelea kufundishwa katika jamii ili watu waepuke ukatili wa kijinsia kwani ni jambo baya.
“Tunaona ni namna gani kesi za ukatili zinavyofika Kanisani au wakati mwingine Misikitini na unakuta ukatili wanaweza kufanyiwa wanawake au ndugu, kwa kweli ukatili unaofanywa haya Mungu uwa hapendezwi nao,”amesema
Amesisitiza kuwa kama wazazi ,viongozi wa dini,viongozi wa serikali wanapaswa kukemea kwa pamoja juu ya ukatili wowote ikiwemo kipigo,kunyimwa haki za msingi, na ukatili wanaofanyiwa watoto kukosa haki zao za msingi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best