Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU),Septemba 12,2024 imekutana na viongozi wa Asasi za Kiraia (AZAKI) na sekta binafsi,ili kuweka mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa hasa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Mwanza, James Ruge,amesisitiza kuwa taasisi hiyo inatambua mchango wa wadau hao katika mapambano dhidi ya rushwa,hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuzuia rushwa katika uchaguzi kwa njia ya elimu, na kwamba lengo ni kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.
Ruge ameongeza kuwa uchaguzi usiozingatia misingi ya haki na uwazi,uchangua kupata viongozi wasio waadilifu ambao hukwamisha maendeleo. Hivyo TAKUKURU imebuni mikakati ya kukabiliana na rushwa kutokana na madhara yake katika jamii.
Amesisitiza mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mtu, na mafunzo hayo yanalenga kuhamasisha ushirikiano wa pamoja katika mapambano hayo kupitia kauli mbiu ya ‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu langu na lako;Tutimize wajibu wetu.’.
Ofisa wa TAKUKURU, Eli Makala, ameeleza umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa,kuwa ni msingi wa uchaguzi mkuu, na kuhimiza wananchi kuchagua viongozi wenye sifa na kuacha vitendo vya rushwa.
Ameonya kuwa maendeleo yanaanzia katika uchaguzi wa serikali za mitaa,hivyo ni muhimu kuchagua viongozi ambao watasimamia miradi ya maendeleo kwa uadilifu.
Naye Mwenyekiti wa AZAKI Mkoa wa Mwanza, Jimmy Luhende, amesema uchaguzi ni eneo lenye changamoto kubwa zinazohusiana na maadili, fedha, urafiki, na udugu.Ambapo amependekeza kuwa elimu kuhusu rushwa ijielekeze kuondoa ujinga katika jamii, kwa kuwa maeneo yenye maendeleo hayakukumbatia rushwa.
Mkurugenzi wa Hope For Youth Development Organisation (HYDO) na Katibu wa AZAKI mkoani Mwanza, Anitha Samson, ameiomba TAKUKURU kupeleka elimu waliyopata kwa jamii ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.
Kwa upande wake Ofisa Uchaguzi Jiji la Mwanza, Lilian Macha amezitaka AZAKI na sekta binafsi, zikatimize wajibu wao wa kikatiba kwa kuwa mabalozi wazuri katika jamii wakachague viongozi watakaowaletea maendeleo kwani ushiriki wao katika mafuno hayo si wa bahati mbaya.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote