May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi ngazi za juu watakiwa kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Chini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

KATIKA kumuunga mkono Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kutatua kero mbalimbali za wananchi viongozi wa ngazi za juu wametakiwa kutoa ushirikiano
kwa watendaji wa ngazi za chini ili kulinda maslahi ya wananchi na ya nchi kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa jijini Dar es salaam hivi karibuni na Diwani wa kata ya minazi mirefu Godlisten Malisa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mambo mbalimbali katika kata hiyo ambapo amesema Rais Samia anateua viongozi kwa ajili ya kumsaidia kutatua chagamoto za wananchi hivyo watendaji wote kwa ujumla wanajukumu la kufanya kazi kwa pamoja pasipo kumuangusha .

“Kwa pamoja tukishirikiana sisi kama watendaji tuliochini ya Rais tuweza kutimiza malengo ya Rais Samia ya kutatua kero za wananchi kupitia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM”amesema Malisa.

Amesema Rais ni Taasisi, na anafanya kazi na watu wengi wakiwemo viongozi mbalimbali hivyo ni vyema kuanzia watendaji wa Mtaa hadi Mkuu wa Mkoa wakasimama kumsaidia Rais na sio kumkwamisha kwa kuzuia maendeleo yasifanyike.

Akizungumzia maendeleo ya kata hiyo, alisema bado kuna changamoto ya ukosefu wa kituo Cha Afya pamoja na Shule ya Msingi jambo ambalo limekua kero kubwa hasa kutokana na ukubwa na wakata hiyo na wananchi waliopo.

Amesema kwa kushirikiana na wananchi wameanza kushangishana fedha kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili, ili kuleta maendeleo ambapo wameshaandika barua kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ili kuomba eneo la kujenga vituo hivyo.

“Kata yetu ina changamoto ya kituo Cha Afya na pamoja na Shule ya Msingi, tumeomba pesa tukipewa kutoka Serikali Kuu tunaweza kuanza ujenzi wowote kati ya hivi vitu viwili, kwa sababu vyote ni muhimu itategemea pesa za ujenzi gani zitaingia mwanzo”amesema Malisa.

Katika hatua nyingine, Diwani huyo, amewaomba wakazi wa Kata hiyo kushirikiana naye katika masuala mbalimbali ili kuweza kuleta maendeleo ndani ya kata hiyo, kwani yeye peke yake hawezi kufanya kila kitu lazima washirikiane .

Kwa upande wa ulinzi na usalama Malisa amesema, katika ofisi za kata Diwani huyo wanapanga kwenda kumshauri Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kuweka utaratibu maalumu kwa wagambo ili kuweza kuondoa vitendo vya rushwa katika majukumu yao.

“Suala la ulinzi ni jambo la msingi sana, ndio maana tunataka tujenge kituo Cha Polisi ili Polisi jamii wawe wanaenda kuripoti kituoni, kuna vitendo viovu vimeanza kujitokeza hii yote imetokana na kukosekana kwa ulinzi kitoimarika”amesema Malisa.

Katika hatua nyingine Diwani huyo amemuomba katibu Mkuu wa Kilimo kushughukulikia suala nzima la Magodauni ya Sudeko ili waweze kupata eneo la kujenga Shule na Kituo cha Afya .