November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania (NEEC), Beng'i Issa Mazana akiambatana na baadhi ya Maafisa wa Serikali kuangalia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na vijana wa Kambi ya Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini (TYC),Mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki.

Vijana watakiwa kuchangamkia fursa nchini

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania (NEEC), Beng’i Issa Mazana amewataka vijana kuhakikisha wanashiriki kiukamilifu fursa mbalimbali katika nchi kwa maendeleo yao binafsi na ya nchi zao kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki mkoani Kilimanjaro wakati wa kufunga Kambi Maalum ya Vijana (Pan African Youth Camp) iliyowakutanisha vijana 50 wanaoleta Mabadiliko Chanya katika Jamii zao Kupitia Miradi yao ya Kijasiriamali na Umiliki wa Makampuni na Viwanda Vidogo Katika nchi za Afrika Mashariki iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini (TYC).

Amesema ni muhimu kuwawezesha vijana na kuwasaidia katika kuwaandaa katika ujasiriamali wao na kuwafanya wanaweza kutekeleza shughuli zao ipasavyo.

“Ninatambua kuwa ninyi vijana wenye uthubutu wa hali ya juu kwani nimejionea kazi zinazotokana na miradi yenu, na naomba niwapongeze sana kwani mnafanya kazi nzuri serikali, itaendelea kutengeneza mazingira wezeshi na rafiki kwa vijana kujifunza pia kuweza kujiajiri ili kukuza uchumi wao binafsi lakini pia kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi,”amesema

Mazana amesema serikali inahitaji kuona vijana wanapata fursa za kujifunza ndani na nje ya nchi na kutumia fursa mbalimbali ambazo zimeajiri vijana wengi ikiwemo sekta ya kilimo na biashara.

“Ni jukumu letu wadau wa maendeleo ya vijana kujenga mazingira wezeshi ikiwemo upatikanaji wa mitaji pamoja na soko la bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi na kutoa mafunzo kwa vijana kwani yatasaidia kuimarisha na kukuza mitaji na biashara zao,”amesema na kuongeza

“Naipongeza Tanzania Youth Coalition (TYC) kwa kufanikisha kambi ya vijana na ninapenda kuwatakia mafanikio mema katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ,nawasihi muweze kutafuta taarifa muhimu za uwezeshaji kwenye tovuti mbalimbali mzitumie kama fursa katika shughuli zenu,”amesema

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini (TYC),Lenin Kazoba amesema kupitia kambi hiyo inawasaidia vijana kupata fursa ya kuweza kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao na taifa.

“Kipindi chote cha siku tano Vijana wamepata wasaa wa kujadiliana changamoto na mafanikio waliyonayo kwa siku tano na kukutana na wataalam kutoka idara mbalimbali ikiwa ni kuwapa nafasi ya kujifunze kutoka kwao ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili na kwenda kuboresha hasa mnachokifanya ili kikaweze kuleta matokeo chanya maradufu ya hapo mlipo,”amesema na kuongesa

“TYC itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajengea uwezo vijana hasa kupitia programu inazotekeleza na kuamini vijana ni mabalozi wazuri wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla hivyo basi nasi tutafanya kila liwezekanalo kushirikiana na idara mbalimbali za serikali katika kuangalia fursa mbalimbali za kuwajengea uwezo vijana wa Tanzania bara na Visiwani,”amesema