December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana waomba vifaa vya michezo

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

SHINA la Wakereketwa la Vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi UVCCM tawi la Sanzale B eneo la Magereza Kata ya Magomeni wameomba kusaidiwa vifaa vya michezo ikiwemo jezi.

Katika taarifa ya tawi iliyosomwa na Rachel Ally ambaye ni mjumbe wa shina mbele ya mgombea Udiwani wa Kata hiyo Mwanaharusi Jarufu aliyeambatana na viongozi mbalimbali, imeelezea changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa uwanja na kukosa vifaa ikiwemo jezi na mipira.

“Sisi vijana wa tawi la Sanzale hapa Magereza Kigongoni tunajihusisha na shughuli za kimichezo baada ya kazi za kila siku, lakini tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa katika mazingira rafiki ha uwanja, hatuna jezi wala mipira,” ameeleza katika taarifa hiyo.

Akijibu changamoto hizo, Jarufu amesema, suala hilo lipo ndani ya uwezo wao hivyo endapo watafanikiwa kupata cheo hicho baada ya kukamilika kwa upigaji kura atalifanyia kazi mapema iwezekanavyo.

“Mimi hapa Sanzale changamoto zenu nalala nazo naamka nazo kwa maana nipo nanyi muda mwingi, niwaahidi kwamba pindi zoezi la upigaji kura likimaalizika na kichaguliwa hili nitalifanyiakazi mapema iwezekanavyo,” amesema Jarufu.

Aidha amewataka vijana hao kujisajili kisheria ili pamoja na shughuli za kimichezo pia wawe na mtaji wa kibiashara, hivyo watumie fursa ya mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri.