Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali ya Mkoa wa Dodoma imewataka vijana, wafanyabiashara, wakandarasi, watoa huduma na wadau wa ununuzi wa umma pamoja na makundi maalum wa mkoa wa Dodoma kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana katika zabuni za Serikali ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa changamoto hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya fursa na haki za wafanyabiashara na makundi maalum katika michakato ya ununuzi wa umma yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha katika sekta ya ununuzi wa umma.
Mhe. Senyamule amesema kuwa Serikali inayaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia mifumo ya ununuzi wa umma inayowezesha wazabuni kushiriki kwa uwazi huku haki zao zikilindwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Ununuzi wa Umma nchini.
Kadhalika, ameipongeza PPAA kwa kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara, vijana na makundi maalum kuhusu fursa zilizopo katika zabuni za umma pamoja na namna ya kushiriki kikamilifu katika michakato hiyo.

Senyamule amesema bado kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili watanzania wengi zaidi wapate uelewa wa sheria za ununuzi wa umma, haki zao pamoja na namna bora ya kushiriki katika zabuni za Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa Vijana, wafanyabiashara na makundi maalum kuhusu haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kushughulikia malalamiko na rufaa.
“Kutokana na maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, PPAA imeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia malalamiko na rufaa kupitia Mfumo wa NeST tangu Februari 2025,” amesema Sando

Sando amesema kuwa matumizi ya Moduli ya kushughulikia Malalamiko na Rufaa katika mfumowa NeST yameleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuokoa muda, kupunguza gharama, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za malalamiko na rufaa zinazowasilishwa na wazabuni.
Sando ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, PPAA imefanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 1,296 pamoja na watumishi 705 wa idara za ununuzi na sheria katika maeneo mbalimbali nchini, huku vijana 878 wakipatiwa mafunzo maalum ya kudai haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma kutoka katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, na Mbeya.
Kadhalika, Sando ameongeza kuwa PPAA ina mpango wa kuunganisha Moduli ya kushughulikia Malalamiko na Rufaa na mfumo wa Mahakama ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma stahiki kwa wananchi kwa wakati kama ilivyosisitizwa katika Dira ya 2050.

More Stories
Itunda: Serikali yaleta mageuzi hospitalini
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi