Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI mkoani Mbeya imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya.
Akizungumza leo Mei 22, 2026 wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya, mkuu wa wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wataalamu wa afya, viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Mbeya.
“Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika sekta ya afya hivyo tuna kila sababu ya kujivunia hatua hii kubwa. Rais Dkt. Samia amefanya kazi kubwa, lazima tuseme ndugu zangu,” amesema Itunda.

Aidha, amesema ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa wauguzi waliojitokeza kusherehekea siku yao, akisisitiza kuwa wauguzi ni uti wa mgongo wa huduma za afya kutokana na mchango wao mkubwa katika kuhudumia jamii.
Itunda amesema juhudi za serikali zimeleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya, ambapo wananchi wengi sasa wanapata huduma kwa urahisi zaidi hata katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, mkazi wa Ilomba, Maria Andrea amesema sekta ya afya imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kuanzia zahanati, vituo vya afya hadi hospitali za rufaa.
“Sasa hivi ukifika hospitali unahudumiwa vizuri hadi unajikuta umepona mapema kabla hata ya tiba….kuanzia wahudumu wa afya hadi madaktari bingwa, kazi yao ni nzuri kweli, hata maboresho ya miundombinu yanaonekana,” amesema Andrea.

More Stories
Vijana ,wafanyabiashara na kundi maalum waaswa kuchangamkia fursa za umma
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi