May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wa BBT awamu ya kwanza wahitimisha mafunzo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Mb) amekutana na kuzungumza na vijana wahitimu wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Bulding A Better Tomorrow – BBT) na kuwapongeza kwa kumaliza salama mafunzo katika Vituo Atamizi vinavyopatikana kwenye Vyuo vya Kilimo vilivyopo sehemu mbalimbali nchini.

Amesema hayo leo Agosti 28, 2023 jijini Dodoma na kuwataka vijana hao kutambua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwawezesha vijana ili kujiinua kimaisha Kwa kujiajiri kupitia kilimo na biashara.

“Nyie vijana 763 ambao mmefikia tamati ya mafunzo ya BBT kati ya 812 mliojiunga na mradi huu mmewasafishia njia vijana wengine watakajiunga na mradi huu katika awamu nyingine na nimeridhishwa sana na nia ya dhati mliyokuwa nayo hadi kufikia tamati,” amesema Bashe.

Waziri Bashe ameongeza kuwa tayari wapo wadau wa maendeleo ambao wamevutuwia na programu ya BBT na tayari imekuwa programu ya kuigwa kwa kuanzisha kwenye nchi zao.

Pia amebainisha kuwa zipo Taasisi za fedha ambazo zimeonesha nia ya kusaidia vijana wa BBT.

“Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia ametembelea BBT na amevutiwa sana na programu hii. Kadhaalika, ujumbe wa nchi za SADC umetembelea BBT Arusha ili kupata taarifa zaidi za kuweza kutengeneza programu hiyo,” ameeleza Waziri Bashe.

Vijana hao wameandaliwa mafunzo maalumu katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kujengewa uzalendo wa kazi na kujua thamani ya uwekezaji wa Serikali kwa vijana.

“Niwatoe hofu marafiki zangu nataka mtambue kuwa huko JKT mtawekewa mpango wa kujengea uwezo zaidi kwenye uzalendo na masuala mengine mtambuka,” amesema Bashe.