Yamo utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, wanyimwa dhamana
Na Grace Gurisha
MAOFISA wanne wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka tisa, yakiwemo ya kughushi, kula njama, utakatishaji fedha na kuisababishia NEMC hasara ya sh. milioni 18.5.
Washitakiwa hao ni Deusdedith Katwale, Lydia Nyinondi ambaye ni Mhasibu Msaidizi wa NEMC, Magori Matiku na Obadia Machupa ambao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Janeth Magoho alidai kati ya Juni Mosi 2016 na Julai 30, 2017 ndani ya jiji la Dar es Salaam na Dodoma, washtakiwa walikula njama ya kutenda makosa ya kughushi, kutoa nyaraka iliyoghushiwa, kuisababishia mamlaka hasara na kutakatisha fedha.
Magoho alidai kati ya Agosti Mosi,2016 na Septemba 6,2016 maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Katwale alighushi ripoti ya kutathmini mazingira ya mradi wa Kituo cha Mafuta cha Ibra General Enterprises lililopo kitabu namba 132 Block T Chadulu Area A Dodoma.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sophia Nyanda alidai katika mashtaka ya tatu kuwa Julai 4,2016 na Julai Mosi,2017 maeneo ya Kinondoni Katwale alighushi nyaraka ya ‘Minutes for Technical Advisory Committee (TAC) kuonesha kwamba kikao hicho kilichofanyika.
Pia alidai Julai 5, 2016 maeneo ya Ofisi za NEMC Kinondoni, Nyinondi alighushi risiti yenye thamani ya sh. milioni 18.5 kuonesha kuwa zimelipwa kwa NEMC.
Katika mashtaka ya tano, ilidaiwa kati ya Juni Mosi, 2016 na Julai 30,2017 katika Ofisi za NEMC Kinondoni, Katwale aliwasilisha nyaraka ya uongo kwa Mkurugenzi wa NEMC kuhusu mradi wa mafuta wa Ibra General Enterprises kuonesha kuwa ukaguzi ulifanyika.
Mwendesha Mashtaka Stanley Luoga, alidai Julai 5,2016, Matiku aliwasilisha nyaraka ya uongo ya risiti kwa Yunis Mfala.
Pia alidai washtakiwa wakiwa watumishi wa NEMC walikiuka kifungu 29 cha Sheria ya Usimamizi Mazingira iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na hivyo, kujipatia Sh milioni 18.5 kwa ajili yao.
Katika mashtaka ya kusababisha hasara, ilidaiwa washtakiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu walisababisha hasara ya sh. milioni 18.5.
Wanadaiwa walijipatia fedha hizo kutoka kwa Mfala ambaye ni mmiliki wa mradi wa kituo cha mafuta cha Ibra General Enterprises wakati wakijua fedha hizo ni haramu na zimetokana na kosa la kughushi.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ametoa kibali cha kusikiliza kesi hiyo.
Wakili wa utetezi, Rugemeleza Nshala alidai wanaomba dhamana kwa wateja wao kwa sababu Mahakama Kuu imeshatoa uamuzi kwamba mashtaka ya utakatishaji fedha yanadhaminika.
Akijibu hoja hiyo, Luoga alidai upande wa mashtaka una pingamizi na dhamana kwani mashtaka ya utakatishaji fedha hayafahamiki na kwamba wanafahamu uwepo wa kesi ya kikatiba ambayo iliamuriwa na Mahakama Kuu.
Alidai mahakama imewapa muda wa miezi 18 Serikali kufanya mabadiliko ya sheria iliyozuia dhamana kwa washtakiwa wa makosa ya utakatishaji fedha kwamba yadhaminike na kabla ya hapo sheria iendelee kutumika kama kawaida.
Hata hivyo, Nshala alidai mahakama inayo mamlaka ya kutoa amri yoyote kuhusu dhamana ambayo ni haki ya kikatiba ya washitakiwa.
Akitoa uamuzi, Hakimu Shaidi amesema licha ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa mashtaka hayo kudhaminiwa lakini pia imetoa masharti kwamba Jamhuri irekebishe sheria hiyo kwa miezi 18.
Amesema maombi hayo ya dhamana kwa sasa si sahihi na kama mtu ataona si uamuzi sahihi aende Mahakama Kuu kwa ajili ya kufanya mapitio.
“Mahakama yangu imefungwa mikono haiwezi kutoa dhamana, hivyo washtakiwa mtaendelea kubaki rumande hadi Juni 18, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali,” amesema Hakimu Shaidi.amesema
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote