January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vigogo Manispaa Kigamboni kuburutwa mahakamani Dar

Wataunganishwa na AG, Mkurugenzi, DC, wapewa notisi ya siku 90, ni
katika sakata la mfanyabiashara maarufu, afikisha kilio chake kwa Rais

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

VIGOGO na baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam wanakusudiwa kuburutwa mahakamani kwa nadai ya kumfutia umiliki wa eneo la shamba mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Iqbal bila hata kumpa notisi ya nia ya Manispaa kulitwaa eneo hilo.

Tayari mfanyabiashara huyo kupitia mawakili wake wameiandikia notisi ya siku 90 Serikali ya kusudio la kuiburuta mahakamani kwa tuhuma hizo.

Miongoni mwa waliotajwa kwenye notisi hiyo kuburutwa mahakamani ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigamboni (sasa DC wa Ilala), Nghilabuzu Ludigija.

Kwa mujibu wa notisi hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake, eneo ambalo mfanyabiashara Iqbal analalamikia kuporwa kwa kufutiwa umiliki wake, lipo Ungindoni, Mji Mwema Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mbali na DC Ludigija, wengine wanaokusudiwa kuburutwa mahakamani ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwanasheria wa manispaa, mtumishi wa Manispaa ya Kigamboni (jina tunalo) na viongozi wengine wa zamani na wa sasa wa Manispaa ya Kigamboni.

Aidha, notisi hiyo imeeleza kwamba wapo wengine kadhaa ambao wataburuzwa mahakamani, ambapo zitatumika taratibu za kisheria kupata taarifa kamili.

Notisi hiyo imetumwa kwa wahusika chini ya vifungu vya 6 (2); 6 (3) na 16 (4) vya Sheria ya Mashtaka yanahoihusisha Serikali (The Government Proceedings Act)(Cap. 5 R.E. 2019), kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Written Laws (Miscellaneous) Amendment Act, 2020 (Act. No.1 of 2020); na kifungu cha 106 (1) (a) cha Sheria ya Local Government (Urban Authorities) Act (Cap.288), kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Written Laws (Miscellaneous) Amendment Act, 2020 (Act. No.1 of 2020).

Aidha, mfanyabiashara huyo amemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan akilalamikia kudhurumiwa haki yake hiyo 

Kwa mujibu wa notisi hiyo mfanyabiashara huyo aliloporwa (kufutiwa umiliki) wa eneo hilo na viongozi hao wakati yeye ndiye alikuwa mmiliki halali baada ya kulinunua kutoka kwa wamiliki wa awali.

Inaeleza kuwa baada ya kununua eneo hilo alilipima na vikapatikana viwanja vilivyopimwa na kutambulika kisheria kama viwanja namba 386, 388, 390, 392, 394-396, 442-446, 448, 450 na 454-562 ambavyo vyote vipo Kitalu (Block) C, kama inavyooneshwa katika Registered Survey Plan No. 40873 ya Agosti 8, mwaka 2005, ambayo wameiambatanisha kama Kielelezo “IMH -1”.

Notisi hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya Lotus Artoneys inaongeza kueleza kwamba; “Siku 90 anazozitoa mteja wetu kwako ni kwa mujibu wa Sheria, ni fursa nzuri kuyatafakari maswali yafuatayo na pengine yajibiwe kwa vile mteja wetu ambaye ndiye mhanga aliyeumizwa na jambo hili hajapewa majibu yake hadi leo”.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Katika Notisi hiyo mfanyabiashara, Iqbal anahoji utaratibu uliotumiwa na Manispaa kufuta umiliki wake katika ardhi hiyo, kutokupewa fursa ya kurekebisha dosari yoyote kama ilikuwepo kwa mujibu wa sheria

Aidha Iqbal, anadai hajui ni kwa nini hakuwahi kupata notisi ya nia ya Manispaa kulitwaa eneo hilo wala hajui kwa nini hakupewa fursa ya kujieleza katika tuhuma au ukiukwaji wowote aliotuhumiwa kuufanya (kama kweli alifanya), kabla hatua nyingine yoyote kuwa imechukuliwa ikiwemo kupokonywa eneo hilo.

Kitendo hicho kimetajwa kwamba kilikuwa cha uonevu na utumiaji mbaya wa madaraka, kwani kinadhihirishwa na ukweli kuwa yapo maeneo mengi wilayani Kigamboni ambayo yalikuwa ama yako katika hali kama ya eneo lake na mengine yasiyoendelezwa kabisa yakaachwa na yeye akawa mlengwa kwa sababu eneo lake lilikuwa lina maendelezo kama nyumba, umeme, kisima na pampu ya maji, ufugaji wa mbuzi, miti iliyooteshwa pamoja na wafanyakazi.

“Lakini pia hata kama tuhuma hizo zingekuwa na chembe yoyote ya ukweli, bado kuna taratibu za kisheria zilizopaswa kufuatwa tofauti na nguvu za ki-imla na ubabe/utumiaji mabavu pasipo kupewa notisi ama haki ya kusikilizwa,” ilieleza notisi hiyo na kuongeza;

“Mteja wetu anaamini pia kuwa uchunguzi wowote ulio huru na wa haki katika uporaji huo haramu wa ardhi yake katika eneo la Ungindoni uliofanywa na maofisa aliowataja wa Manispaa ya Kigamboni, utabaini pia dhuluma nyingine nyingi alizowahi kufanyiwa pia katika maeneo mengine mengi tofauti aliyowahi kumiliki ndani ya wilaya ya Kigamboni.”

“Mteja wetu anaamini kwa dhati kuwa Notisi hii ya siku 90 tunayoileta Serikalini leo ni fursa adhimu kwa watendaji Serikalini (Manispaa ya Kigamboni, mkoa wa Dar es Salaam na hata Ofisi ya Mwanasheria Mkuu) kulifanyia kazi na kulitatua kiungwana,” ilisisitiza.