Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online
VITENDO vya uhalifu uliohalalishwa na wakazi wa eneo la Kijijini, Mbezi Beach B, Kawe jijini Dar es Salaam, viliripotiwa na Gazeti la Majira, juzi vimewafanya viongozi mbalimbali kufika eneo hilo ili kujionea uhalisia wa yale yanayoendelea.
Miongoni mwa vitendo vya uhalifu vinavyofanyika eneo hilo ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji bangi, unywaji pombe haramu na ngono za nipe nikupe (kununua).
Habari za kuaminika ambazo gazeti hili limezipata zimeeleza kwamba, baada ya gazeti hili, kuripoti taarifa za uhalifu huo, uliohalalishwa na wakazi hao viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Saad Mtambule walifika kujionea yanayojiri, eneo hilo.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari vigogo wengine ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Katibu wa Wilaya ya kinondoni na wengine.
“Kwenye msafara huo walikuwepo viongozi kuanzia ngazi ya kata na wilaya kwa ngazi zote,” alisema mtoa habari wetu na kulipongeza Gazeti la Majira akisema limefanyakazi kubwa ya kuibua uozo uliokuwa unafanyika eneo hilo.
Alisema wanachotegemea sasa ni kwamba tatizo hilo litapata ufumbuzi kwani watoto wao wamekuwa hatarini.
Kwa upande wake DC, Mtambule alisema ni kweli wameona eneo hilo na kuna jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.
Aidha, chanzo chetu kutoka Mamlaka ya Kuthibiti Dawa za Kulevya (DCEA) kimeeleza kwamba kutokana na taarifa iliyoripotiwa na Majira, mamlaka hiyo itaenda kulifanyia kazi eneo.
“Kutokana na hiyo taarifa mamlaka itabidi kwenda kulifanyia kazi eneo hilo,”kilisema chanzo chetu cha habari.
Tangu kuripotiwa yanayoendelea eneo hilo, wakazi wa eneo wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi hasa kutokana na ziara zinazofanywa na viongozi katika eneo hilo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa baadhi yao wameficha dawa za kulevya, bangi na pombe haramu kwenye bustani zao za mboga za majani zilizopo jirani na eneo hilo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato