May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mbwanji:Watumishi toeni elimu umuhimu wa mazoezi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WATUMISHI wa Idara ya Tiba Mazoezi wa jengo jipya katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Mbeya wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya lazima.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ,Dkt.Godlove Mbwanji wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la tiba Mazoezi lililopo katika hospitali hiyo.

Dkt.Mbwanji ameushukuru uongozi wa hospitali pamoja kamati yote iliyofanikisha kukamilika kwa jengo hilo pamoja na ushirikiano ulioonyeshwa na watumishi wa hospitali akiwemo Mhandisi alisiyesimamia shughuli zote za ujenzi huo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa jengo hilo litapanua wigo wa upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa wenye matatizo ya maumivu ya viungo.

“.Na mimi naomba shukrani zote nilizopewa ni za uongozi wa hospitali na watumishi wote kwasababu vyote vilivyofanyika ni watumishi wamefanya kazi kupitia sehemu ya mapato yanayopatikana..” Dkt Mbwanji

Seraphine Mushi ni Mkuu wa Idara ya Fiziotherapia hospitalini hapa, ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya chini ya Dkt. Mbwaji kupitia maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika idara hiyo ikiwemo ongezeko la vifaa tiba pamoja na upanuzi wa jengo hilo ambapo hapo awali lilikuwa na uwezo kuhudumia wagonjwa wa nje 30 hadi 40 kwa siku na sasa lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 120 hadi 200 kwa siku.

“Hapo awali jengo hili lilikuwa na vyumba 16 vya matibabu na sasa vimeongezeka vyumba nane pamoja na eneo la kufanyia mazoezi ambavyo vitapelekea uwezo wa kutibu wagongwa wa nje 120 hadi 200 kwa siku ukilinganisha na zamani tulikuwa tukiona wagonjwa 30 hadi 40 kwa siku,” Seraphine Mushi.

Mathias Mkoma, Revocatus Zege na Mitreni Sichembe ni wagonjwa wanaopatiwa huduma ya matibabu kwa njia ya tiba mazoezi Hospitali hapo wamepongeza uongozi wa hospitali pamoja na watumishi wa idara hiyo kutokana na huduma wanazopatiwa katika kipindi chote cha huduma.

“Tumefurahishwa sana na huduma zinazopatikana katika idara hii hivyo hatuna budi kuupongeza sana uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, wahudumu wote pamoja na madaktari kwa kweli wanafanya kazi kwa upendo sana”wamesema.

Katika hafla hiyo pia watumishi kutoka idara ya Fiziotherapia walipata nafasi ya kumkabidhi Cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji kama ishara ya kutambua mchango wake kutokana na ushirikiano mkubwa anao uonyesha katika jitihada mbalimbali za kuboresha huduma hospitalini hapo kitendo kilichoambatana na zoezi la ukukataji wa keki kama ishara ya pongezi.