Na Irene Clemence, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema imejipanga kuongeza idadi ya usajili wa wanafunzi kutoka 704,000 na kufikia 1,000,000 ifikapo 2021/2022 ili kuzalisha wabunifu wengi zaidi katika nyanja mbalimbali.
Akizungumza katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Peter Sitta amesema, lengo lao kubwa ni kuhakikisha inawajengea uwezo na umahiri wa kutosha ili waweze kuwa na ubunifu wa kubuni vitu mbalimbali.
Sitta amesema, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilitoa jumla ya Sh. bilioni 40 kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Fundi Stadi (VETA), kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi na upanuzi wa vyuo 40 vikiwamo vipya 25.
“VETA imejenga miradi 10 ya ujenzi wa vyuo katika Halmashauri ya Nkasi Rukwa, Ireje Songwe, Kasulu Kigoma ambapo katika vyuo hivi tunashiriki kutoa nguvu kazi yetu,”alisema Sitta.
Akizungumza Maonesho ya mwaka huu, Sitta amesema wamefanikiwa kuja na teknolojia mpya 12 zikiwamo mashine ya ubuyu, kuchemsha maji pasipo kutumia umeme, mfumo wa kunawa maji bila koki.
Teknolojia nyingine ni pamoja na kuingiza umeme mita ukiwa mbali, ushonaji wa kidigitali, mashine ya kupanda mazao, ukaushaji bora mazao ya Samaki na nishati ya umeme pasipo chanzo cha mafuta wala maji.
Pia teknolojia ipo teknolojia ya kuchenjua madini kutoka kwenye madini pasipo kutumia zebaki, ubunifu wa samaki kikiwamo kitanda tiba na kochi.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote