



Na Jouce Kasiki, Rukwa
SERIKALI imeongeza kiwango cha fedha zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya mikopo na uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15, kuanzia mwaka wa fedha 2026/27, hatua inayolenga kupanua fursa za kiuchumi kwa makundi hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema hayo Oktoba 10 2026 alipomwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika ufunguzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa 2026, inayofanyika mjini Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.
Profesa Mkenda amesema Serikali inalenga kuhakikisha vijana, wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu, wanapata fursa sawa za mitaji, elimu ya ujasiriamali na ushiriki katika shughuli za kiuchumi, bila kujali mazingira wanayotoka.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ujuzi kupitia taasisi za mafunzo ya ufundi, ikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili kuwaandaa vijana kupata ajira na kujiajiri kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
Amesisitiza kuwa vijana wanahitaji zaidi ya vyeti vya elimu, bali pia ujuzi wa vitendo, uwezo wa kutatua changamoto, kutumia teknolojia na kuanzisha shughuli za uzalishaji zitakazowawezesha kujipatia kipato.
Akizungumzia fursa za uwezeshaji, Profesa Mkenda amesema vikundi 299 vya vijana vyenye wanachama 2,226 vilikuwa vimepata zabuni za Serikali zenye thamani ya Sh bilioni 13.2 kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha katika hotuba yake.
Ameyataja mashirika na taasisi za Serikali kuendelea kutoa elimu na kuwawezesha vijana kuingia katika mfumo wa zabuni za umma ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, mifumo ya kidijitali ya upatikanaji wa taarifa za fursa na programu za mafunzo ya biashara ili kuhakikisha vijana wanapata mitaji inayoambatana na ushauri, masoko na ujuzi wa kusimamia miradi.
Akizungumzia hali ya ajira, Profesa Mkenda alisema takwimu za Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi zinaonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kilipungua kutoka asilimia 8.3 mwaka 2024 hadi asilimia 7.5 mwaka 2025.
Hata hivyo, amesema bado kuna umuhimu wa kuongeza ajira zenye tija na kuwaandaa vijana kukabiliana na mabadiliko ya soko la ajira yanayochochewa na maendeleo ya teknolojia, akili unde, kilimo cha kisasa na biashara za kidijitali.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na vijana 21,312,411 wenye umri wa miaka 15 hadi 35, sawa na asilimia 34.5 ya watu wote nchini, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwekeza katika kundi hilo kwa maendeleo ya Taifa.
Profesa Mkenda amezitaka Halmashauri kuhakikisha taarifa za mikopo, mafunzo na fursa za biashara zinawafikia vijana katika ngazi za kata, vijiji na mitaa. Alisisitiza pia umuhimu wa kuunganisha mikopo na huduma za ushauri wa biashara, teknolojia na upatikanaji wa masoko.
Pia amewahimiza vijana kutumia mifumo rasmi kutafuta fursa, kuandaa miradi yenye tija, kusimamia fedha kwa nidhamu na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha wanufaika wengine kupata huduma hizo.
Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 inafanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 14 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”
Maadhimisho hayo yanalenga kuwakutanisha vijana, Serikali na wadau wa maendeleo kujadili changamoto, kutambua fursa na kuimarisha ushiriki wa vijana katika maendeleo ya Taifa.

More Stories
Yas yawatambua vinara wiki ya huduma kwa wateja
EWURA yaeleza sababu kutangaza bei za mafuta
Kampeni ‘Ongea na Kamanda’ yazinduliwa Mwanza