December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UTPC kuwawezesha waandishi kuondokana na utegemezi

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Dodoma

Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), imedhamiria kuzijengea uwezo Klabu za Waandishi wa Habari mikoani kuwezesha waandishi kuondokana na utegemezi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya jijini Dodoma katika maonesho ya Klabu za Waandishi wa Habari kutoka mikoa 28 nchini ambazo zilionesha mikakati na shughuli mbalimbali za kuwawezesha waandishi wa habari katika mikoa yao kuachana na utegemezi.

Ambapo amesema wakijitegemea na kijisimamia wao watazitendea haki taarifa wanazozitoa kwa kuwa watakuwa huru.

Ameishukuru nchi ya Sweden kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania kwa kuendelea kuzifadhili klabu za waandishi wa habari na kuhakikisha kuwa klabu hizo zinafikia hatua za kujitegemea.

“Ubalozi wa Sweden umetufadhili kwa muda mrefu, tunaushukuru kwa kutujengea uwezo umetufadhili bila kuchoka hadi sasa mpaka tunaelekea hatua ya kutaka kujitegemea ni jambo jema,”amesisitiza Simbaya.

Kwa upande wake Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo amesema waandishi wa habari nchini wameanza safari nzuri kuelekea kujitegemea kiuchumi na kuwa huru kuandika habari zenye kuleta mabadiliko katika jamii ya watanzania.

Baadhi ya mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa miradi ya maendeleo kwa waaandishi wa habari kupitia klabu hizo ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyama vya akiba na mikopo(SACCOS), VIKOBA, miradi ya kilimo, miradi ya habari za uchunguzi, biashara na miradi ya vifaa vya uandishi wa habari.

Katika maonesho hayo baadhi ya viongozi wa klabu hizo walionesha mikakati ya kumiliki vyombo vya habari vya klabu, redio, magazeti,televisheni na mitandao ya kijamii jambo ambalo Sonkolo amesema ni hatua kubwa katika tasnia ya habari nchini.

Ambapo amesema maonesho ya mwaka huu yamewapa picha kwamba wanaweza kuinua hali ya uchumi ya waandishi kote nchini kupitia klabu zao za mikoani hivyo mwaka kesho watafanya maonesho makubwa zaidi kwa sababu hawatakuwa peke yao watashirikisha wadau wengine wanaoshirikiana nao.

“Nitumie fursa hii kusema kuwa mikakati hii iliyowekwa na klabu zetu za kuiondoa UTPC kutoka pazuri na kwenda pazuri zaidi ni hatua nzuri ya kuwainua waandishi wa habari kiuchumi……..,waandishi wa habari watakapokua kiuchumi watakawa huru kuandika habari za kiuchunguzi zenye matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa,”amesema Nsokolo.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa klabu 28 za waaandishi wa habari nchini, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam(DCPC), Samson Kamalalo amewataka viongozi wa klabu za waandishi wa habari kusimamia mikakati yao ili kuzijenga klabu zao.