May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Baraza la wawakilishi Zanzibar awapa pole wana Hanang’

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Maulid amepongeza kazi iliyofanywa na Serikali na Wananchi waliojitolea kusaidia Waathirika wa maafa ya maporomoko ya mawe na tope kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara.

Maulid ametoa pongezi hizo alipoongoza ujumbe kutoka baraza la wawakilishi kutoa Msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa maporomoko hayo katika Halmashauri ya wilaya ya hanang yaliyotokea Disemba 3, 2023.

Ameeleza kwamba, jambo hilo limeonesha kiasi gani nchi ina umoja hususan tunapopata matatizo na namna gani tunashirikiana kama ndugu kulitatua.

“Tumekuja tumeleta kiasi cha shilingi milllioni 30 tunajua mahitaji ni makubwa lakini kidogo kidogo, tukiunganisha nguvu zetu jambo litakuwa kubwa ili isaidie waathirika, “amebainisha.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu  Jenista Mhagama amewashukuru, baraza la wawakilishi kwa msaada wa kibinadamu walioutoa kwa waathirika.

“Jambo hili limeonesha kwamba Muungano wetu si Muungano wa maneno bali ni Muungano  wa vitendo,”amesema Waziri Mhagama

Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kuratibu vyema suala hilo na kuhakikisha kila mchango unatumika kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo na kuongezea kwamba watadhibiti kila mianya ya ubadhilifu na kusisitiza kuwa kwa yeyote atakayefuja michango hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.