December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utoaji mimba usio salama wachangia vifo vya wanawake

Na Stella Aron,TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa utoaji mimba usio salama unachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya uzazi duniani, unafanyika nje ya taratibu za hospitali, kliniki na upasuaji, au bila kuwa na wataalamu wa kitabibu wenye sifa.

Akizungumzia changamoto hiyo daktari Bingwa katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, Dkt.Peter Kibacha alisema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi lakini bado kuna changamoto katika suala la utoaji mimba usio salama ambao huchangia tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.

“Kuna mimba milioni 20 zisizotarajiwa ambazo hutolewa kwa njia isiyo salama duniani hususani katika nchi zisizoendelea kwa kila mwaka hili ni tatizo kubwa.

“Kila mwaka kuna mimba milioni moja zisizotarajiwa na kati yake asilimia 39 huharibiwa kutokana na changamoto hiyo husababisha wasichana na wanawake kupata maumivu makali.

“Kutokana na kitendo hicho huchangia athari kama mlango wa uzazi kushindwa kuhimili na mimba kuharibika na hata kuharibu kizazi au mimba kutunga nje ya kizazi hivyo elimu itasaidia kupunguza utoaji mimba ambao si salama,” alisema Kibacha.

Daktari Kibacha alisema kuwa ili kupunguza ongezeko la utoaji mimba ni vyema sekta ya habari kwa kusaidiani na Serikali na asasi ziziso za kiserikali (NGOs), kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari zitokanazo na utoaji mimba usio salama nchini.

Daktari Kibacha alisema kuna baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikichangia vifo vya wajawazito kama kifafa cha mimba,utoaji mimba usio salama,uvujaji damu usio wa kawaida ambapo Serikali inafanya jitihada kubwa katika kupunguza athari hizo.

“Asilimia 50 ya mimba zisizo tarajiwa hutolewa kwa njia ambayo si salama kutokana na kutumika kwa vifaa ambavyo si salama kama,” alisema.

Naye Mwanasheria Julius Titus, alisema kuwa sheria zilizowekwa nchini zinazohusiana na mfumo wa udhibiti wa haki ya afya ya uzazi ikiwemo sheria ya Makosa ya Jinai inayotoa adhabu kali kwa wale wote wanaojihusisha na utoaji mimba usio salama.

“Ni kweli sheria hii inatambua kuwa mtu anaweza kutolewa mimba endapo itahitajika kunusuru maisha yake, lakini pia inadhibiti utoaji mimba usio salama kwa kutoa adhabu kali ikiwemo kwa mtu atakaye mtoa mimba mwanamke atakabiliwa na adhabu ya miaka 14, atakaye saidia au kutoa nyezo wakati akijua zinakwenda kutumika kwenye utoaji atakuwa na kifungo cha miaka 3. Wakati mwanamke atakaye jaribu kutoa ikidhibitika atakuwa na adhabu ya miaka 7.

“Hatuna sheria za afya ya uzazi ambayo inatambulika kama zilivyo sheria nyingi, mfano sheria ya kazi, ndoa, na aridhi.Bali mambo ya afya ya uzazi yameongelewa kwenye sheria ya makosa ya jinai penal code CAP 16, na miongozo au sera mbalimbali zilizo pitishwa na wizara ya afya ili kutoa mwongozo na kuondoa athari zinazoweza kujitokeza” alisema