December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti wa mbegu watakiwa kuzingatia hali ya hewa

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline, Dodoma.

WATAFITI wa masuala ya kilimo nchini wametakiwa kutumia matokeo ya utafiti wao wanaofanya  katika kuboresha mbegu bora za mazao zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi ili  kuwa na tija katika sekta .

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Desemba 14,2022 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakati akifungua  warsha ya kuelimisha wadau kuhusu Kazi za Muunganiko wa Taasisi za Kimataifa za Utafiti wa Kilimo (CGIAR) .

Dkt. Jingu amesema  lengo kuu la warsha hiyo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kuboresha uratibu wa miradi ya OneCGIAR kwa kuzingatia utafiti utakaongeza uzalishaji.

“Kupitia Mkakati  wa Utafiti na Ubunifu wa Mwaka 2030  CGIAR imeanzisha   mkakati unaojulikana kama OneCGIAR ambao unalenga kufanya utafiti na maendeleo sasa ili tukuze sekta zetu za kilimo, mifugo na uvuvi lazima tuwekeze katika utafiti na maendeleo hivyo  mkakati huu utasaidia katika uzalishaji na tija,” Amesema Katibu Mkuu huyo.

Pia amehimiza kwamba utafiti wa mbegu unaofanyika  usaidie  kuleta tija na faida katika shughuli za wakulima, wavuvi na wafugaji pamoja na kuendeleza ugunduzi wa mbegu mpya hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa.

“Hivi karibuni  kumekuwa na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo utafiti tunaoufanya uendane na hali ya hewa ya kipindi husika ukizingatia  sasa hivi misimu ya mvua imebadilika  kwahiyo tunahitaji mbegu zinazoendana na mazingira na namna ya kukabiliana na wadudu waharibifu,”Ameeleza .

Katika hatua nyingine amesisitiza ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo akisema licha ya uwepo wa sekta zingine kilimo kitaweza kustawi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi endapo vijana watawezeshwa kikamilifu.

“Vijana ili washiriki vizuri  kilimo wanahitaji elimu , mafunzo kwa vitendo na namna ya kutumia fursa ya ukuaji wa teknolojia katika shughuli zao za uzalishaji wenye matokeo chanya na wafanye kwa tija itasaidia vijana kujikwamua kiuchumi wao wenyewe na kushiriki katika pato la Taifa,”Amesisistza Dkt. Jingu.

Aidha ameshauri uwepo wa ushirikiano kati ya Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo kwa kuanzisha miradi mikubwa itakayoleta matokeo chanya  katika sekta hizo muhimu kupitia mkakati huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Dk. Geoffrey Mkamilo  amebainisha kwamba kufanyika kwa utafiti wa mbegu kunasaidia kubaini hali ya mbegu, changamoto na namna ya kuboresha uzalishaji wake utakaoendana na kipindi husika.

“Warsha hii inatuweka pamoja kama wataalamu na wizara za kisekta kubalishana uzoefu na namna ya kufanya utafiti wenye manufaa katika sekta zote za kilimo. Mifugo na uvuvi kubaini mbegu bora na wakati husika wa kuzifanyia kazi ziweze kuzalisha mazao bora kwa jili ya kuimarisha lishe na kipato,”ameeleza Mkurugenzi.

Naye Mtaalamu kutoka OneCGIAR Dkt. Regina Kapinga alifafanua kwamba licha ya kufanya utafiti unaowezesha mazao kuhimili mabadiliko ya tabia nchi pia unazingatia uboreshaji wa virutubishi katika mazao ya uvuvi, mifugo na mimea.