May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

URA Saccos yatoa mikopo ya zaidi ya Bil 400 kwa wanachama wake

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

CHAMA cha kuweka na kukopa cha Usalama wa Raia (URA) Saccos kimetoa mikopo ya zaidi ya sh bil 458 kwa wanachama wake 45,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mkuu Msaidizi wa chama hicho Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Peter Msuya alipokuwa ahojiwa na vyombo vya habari katika maonesho ya siku ya Ushirika Duniani (SUD) yanayoendelea katika viwanja vya nane nane Ipuli mjini Tabora.

Alisema chama hicho ambacho wanachama wake ni askari polisi na familia zao kimewawezesha kujenga nyumba zao, kusomesha watoto, kununua vyombo vya usafiri na faida nyinginezo.

Aliongeza kuwa mbali na kunufaika na mikopo chama hicho pia kimekuza uchumi wao na kuongeza mzunguko wa fedha miongoni mwa jamii.

Afande Msuya alibainisha kuwa chama hicho hadi sasa kina rasilimali zenye thamani ya sh bil 117 na kimeweza kupata tuzo ya ubora kutokana na usimamizi mzuri na uendeshaji wenye tija kwa wanachama wake.

Alifafanua kuwa kwa mwaka jana pekee kimetoa mikopo 17,458 yenye thamani ya sh bil 108.7 kiwango ambacho ni kikubwa kutolewa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006.

DC wa wilaya ya Kaliua Dkt. Rashid Chuachua akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Dk Batilda Burian alipongeza Saccos hiyo kwa kutoa mikopo yenye tija kwa wanachama wake ambao ni watumishi wa Jeshi la Polisi.

Alipongeza serikali kwa kutoa fursa kwa mkoa huo kuandaa maonesho hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo na kubainisha kuwa wapo tayari kuendelea kuyandaa hata mwakani kwa sababu yana manufaa makubwa kwa wananchi wake.

Katika maadhimisho hayo yanayotarajia kufungwa Julai 1, 2023, kumekuwa na mahudhurio makubwa sana ya makundi ya kijamii, wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, vyama vya ushirika kutoka mikoa yote nchini na wadau mbalimbali, na hadi sasa kuna mabanda ya maonesho yapatayo 250.