Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
UONGIZI wa Shirikisho la Machinga (SHIUMA) umewatahadharisha Umma wa Watanzania wakiwemo wanachama wa shirikisho hilo kuhusu watu wanaojifanya kuwa viongozi wa Shirikisho hilo wakati hawana uhalali wowote katika nyadhifa wanazojitambulisha.
Aidha uongozi huo umewasihi wadau na Taasisi mbalimbali za kifedha kutoshirikiana na kikundi hicho wala kutojihusisha na shughuli za watu hao kwani hawatambuliki na Shirikisho hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ,Mwenyekiti Shirikisho hilo Taifa Ernest Masanja amesema,kumekuwa na baadhi ya watu wanaojitambulisha wao ni viongozi wa Machinga Taifa bila uhalali wowote.
Masanja amesema,kikundi hicho cha watu wachache kinachojifanya ni viongozi wa SHIUMA kilivuliwa madaraka hayo kutokana na utovu wa nidhamu na kwamba kwa sasa hawatambuliki kama viongozi wa SHIUMA.
“Leo tunatoa tamko kwamba SHIUMA haitambui wala haihusiki na kikundi cha watu wanaojitambulisha kama viongozi wa SHIUMA bila uhalali wa nyadhifa wanazozitaja ikiwemo kumiliki Machinga Saccos LTD, Gazeti la Machinga na kudai kumiliki taasisi inayotambulishwa kama “Machinga Media Group”.amesema Masanja
Amewataja watu hao wanaojitambulisha kuwa ni viongozi wa SHIUMA ni Lusinde Steven-anayejitambulisha kama Mwenyekiti SHIUMA Taifa,Yusuph Namoto anayejitambulisha kama Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa – Dar es Salaam,Augustino Choja anayejitambulisha kama Naibu Katibu Mkoa wa Dar es Salaam na Mohamed Nchigamo anayejitambulisha kama Mweka Hazina Mkoa wa Dar Es Salaam.
Viongozi wengine ambao hawahusiki na SHIUMA ni Masoud Chauka anayejitambulisha kama Katibu wa Mkoa wa Dar Es Salaam,Shaban Matwebe anayejitambulisha kama mshauri wa machinga Dar es Salaam.
“Watu hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakijishirikisha na vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya chama vilivyosababisha Mkutano Mkuu wa SHIUMA kuwavua madaraka kupitia maazimio ya wajumbe waliokutana Jijini Dodoma 19 Mei, 2022.
Mkutano huo pia uliweka viongozi wa mpito katika nafasi hizo hadi uchaguzi Mkuu utakapofanyika huku akisema viongozi walioteuliwa kuongoza mkoa wa Dar es Salaam ni Christopher Kidiga -Mwenyekiti,John Mbagwile – Makamu Mwenyekiti na Marcelina Mijingo ambaye ni Katibu .
Wengine ni Kelvin Josephat- Naibu Katibu Mkuu ,Mohamed Aali Mweka Hazina , na Ismail Faisal Afisa Habari/Msemaji wa Machinga Dar Es Salaam.
“Kwa tamko hili natarajia Umma wa Watanzania utatoa ushirikiano kwa SHIUMA ili kukidhi matakwa na maono ya viongozi wetu Wakuu waliotuwekea mazingira mazuri kwa mstakabali wa Taifa.”amesisitiza Masanja
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best