May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uongozi wa Machinga watahadharisha wadau kuhusu wanaojifanya viongozi wa Machinga Taifa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

UONGIZI wa Shirikisho la Machinga (SHIUMA) umewatahadharisha Umma wa Watanzania wakiwemo wanachama wa shirikisho hilo kuhusu watu wanaojifanya kuwa viongozi wa Shirikisho hilo wakati hawana uhalali wowote katika nyadhifa wanazojitambulisha.

Aidha uongozi huo umewasihi wadau na Taasisi mbalimbali za kifedha kutoshirikiana na kikundi hicho wala kutojihusisha na shughuli za watu hao kwani hawatambuliki na Shirikisho hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ,Mwenyekiti Shirikisho hilo Taifa Ernest Masanja amesema,kumekuwa na baadhi ya watu wanaojitambulisha wao ni viongozi wa Machinga Taifa bila uhalali wowote.

Masanja amesema,kikundi hicho cha watu wachache kinachojifanya ni viongozi wa SHIUMA  kilivuliwa madaraka hayo kutokana na utovu wa nidhamu na kwamba kwa sasa hawatambuliki kama viongozi wa SHIUMA.

“Leo tunatoa tamko kwamba SHIUMA haitambui wala  haihusiki na kikundi cha watu wanaojitambulisha kama viongozi wa SHIUMA bila uhalali wa nyadhifa wanazozitaja ikiwemo kumiliki Machinga Saccos LTD, Gazeti la Machinga na kudai kumiliki taasisi inayotambulishwa kama “Machinga Media Group”.amesema Masanja

Amewataja watu hao wanaojitambulisha kuwa ni viongozi wa SHIUMA ni Lusinde Steven-anayejitambulisha kama Mwenyekiti SHIUMA Taifa,Yusuph Namoto anayejitambulisha kama Mwenyekiti wa SHIUMA  Mkoa – Dar es Salaam,Augustino Choja anayejitambulisha kama Naibu Katibu Mkoa wa Dar es Salaam na Mohamed Nchigamo anayejitambulisha kama Mweka Hazina Mkoa wa Dar Es Salaam.

Viongozi wengine ambao hawahusiki na SHIUMA ni Masoud Chauka        anayejitambulisha kama Katibu wa Mkoa wa Dar Es Salaam,Shaban Matwebe anayejitambulisha kama mshauri wa  machinga Dar es Salaam.

“Watu hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakijishirikisha na vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya chama vilivyosababisha Mkutano Mkuu wa SHIUMA kuwavua madaraka kupitia maazimio ya wajumbe waliokutana Jijini Dodoma 19 Mei, 2022.

Mkutano huo pia uliweka viongozi wa mpito katika nafasi hizo hadi uchaguzi Mkuu utakapofanyika huku akisema viongozi walioteuliwa kuongoza mkoa wa Dar es Salaam ni   Christopher Kidiga   -Mwenyekiti,John Mbagwile – Makamu Mwenyekiti na Marcelina Mijingo        ambaye ni Katibu .

Wengine ni Kelvin Josephat- Naibu Katibu Mkuu ,Mohamed  Aali Mweka Hazina , na Ismail Faisal Afisa Habari/Msemaji wa Machinga Dar Es Salaam.

“Kwa tamko hili natarajia Umma wa Watanzania utatoa ushirikiano kwa SHIUMA ili kukidhi matakwa na maono ya viongozi wetu Wakuu waliotuwekea mazingira mazuri kwa mstakabali wa Taifa.”amesisitiza Masanja