April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Picha ya marehemu Edward Terso wakati wa uhai wake. (Picha na EYEredio).

UNESCO yamlilia mwanahabari nguli wa Sudani Kusini

JUBA, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetoa salamu za rambirambi kwa familia, marafiki,wanahabari wa vyombo vya habari vya Sudan Kusini kwa kuondokewa na mwenzao, Edward Terso ambaye ni mwanzilishi na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Waandishi wa Habari wa Sudani Kusini (UJOSS).

Kwa mujibu wa UNESCO, wakati wa uhai wake, Terso alitimiza jukumu kubwa la kuwaunganisha waandishi wa habari nchini humo.

UNESCO imeeleza kuwa,marehemu Edward Terso, alikuwa mstari wa mbele katika kukuza uhuru wa waandishi wa habari, upatikanaji wa habari na usalama wa waandishi wa habari huko Sudani Kusini.

Pia kwa muijibu wa UNESCO, kujitolea kwa marehemu katika kazi hiyo kwa miaka mingi kuliwezesha ukuaji wa tasnia ya habari nchini Sudani Kusini.

Aidha, UNESCO imebainisha kuwa, marehemu Edward atakumbukwa kwa kujitolea kwake katika kuandaa sheria za vyombo vya habari vya Sudani Kusini, utetezi wake kwa kuridhia na utekelezaji, ambao ulichangia uboreshaji wa mazingira ya kufanya kazi ya vyombo vya habari nchini Sudani Kusini.

Kwa miaka mingi, marehemu Edward aliwakilisha waandishi wa habari wa Sudani Kusini katika mikutano mbalimbali ya UNESCO, kimataifa, kikanda na kitaifa, ambapo alitetea kitaalam shida za waandishi wa habari na wafanyakazi wengine wa vyombo vya habari nchini mwake.

Pia alikuwa na jukumu kubwa katika kuanzisha na kufanikiwa kuratibu mshikamano wa waandishi wa habari ili kufanya kazi kwa ufanisi nchini Sudan Kusini.

UNESCO imebainisha kuwa,marehemu atakumbukwa kwa jukumu lake kubwa katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari kupitia mafunzo yaliyokusudiwa, kukuza kanuni za maadili kati ya waandishi wa habari na kuongeza uwezo wa UJOSS wa kuangalia na kuripoti ukiukaji wa uhuru wa waandishi wa habari.

Aidha, marehemu Edward alipigania na kukuza uhusiano bora wa kufanya kazi kwa kushirikiana na makundi mbalimbali nchini humo.

Katika nyakati ambazo waandishi wa habari walikuwa wameshambuliwa na vyumba vya habari kufungwa, alichagua mazungumzo badala ya malumbano kati ya waandishi wa habari, wafanyakazi wa usalama na taasisi za Serikali zilizopewa jukumu la kukuza usalama wa waandishi wa habari nchini.

“UNESCO inasikitishwa na kifo hiki cha mwandishi wa habari mashuhuri na mtetezi wa uhuru wa waandishi wa habari na inahimiza ushirika wa Vyombo vya Habari vya Sudani Kusini kumheshimu kwa kuendelea kumuenzi marehemu Edward Terso.Kumbukumbu zake zitabaki kwetu sisi na roho yake inapumzika kwa amani,”imeeleza UNESCO.