May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulenge: Tanzania imeshirikisha vijana kutunga sheria, kulinda amani

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM) Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesema Serikali ya Tanzania imetoa fursa kubwa kwa vijana kwa kushirikishwa kwenye uongozi, utungaji wa sheria na miongozo mbalimbali.

Aliyasema hayo Machi 14, 2023 kwenye Bunge la Dunia kupitia Jukwaa la Wabunge Vijana wa IPU linalofanyika nchini Bahrain, na kuongeza kuwa vijana ni nyenzo kubwa ya kuimarisha amani ya Dunia.

Mhandisi Ulenge alisema kuwa Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa vijana katika maendeleo ya Taifa tangu Uhuru mpaka sasa, hivyo hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhakikisha vijana wanashirikishwa katika kudumisha amani ya nchi zikiwemo utungaji wa sheria na miongozo mbalimbali.

“Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa vijana katika maendeleo ya Taifa letu tangu Uhuru mpaka sasa. Na pia hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhakikisha vijana wanashirikishwa katika kudumisha amani ya nchi zikiwemo utungaji wa sheria na miongozo mbalimbali” alisema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge aliongeza kuwa vijana wakitumiwa vizuri wanaweza kudumisha amani ya Dunia na kuwa na jamii jumuishi na kuweza kuishi kwa kuvumiliana.

“Kama vijana watashirikishwa katika nyanja zote, naona kabisa namna vijana wanavyoweza kudumisha amani na jamii jumuishi na kuweza kujenga utamaduni wa kuvumiliana” alisema Mhandisi Ulenge.

Katika mkutano huo wa Bunge la Dunia, kwa nyakati tofauti, Mhandisi Ulenge amechangia mambo mbalimbali ikiwemo suala la Mabadiliko ya Tabianchi, huku akitetea Hoja ya Dharura iliyowasilishwa na Tanzania kwa niaba ya Umoja wa Nchi za Afrika (AU) ya kutaka kuwepo kwa Mfuko utakaosaidia nchi zitakazopata majanga yatokanayo na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund).

Lakini pia, Mhandisi Ulenge ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) uweke kipaumbele katika miundombonu ya kidigitali ambayo italinda mifumo dhidi ya mashambulizi na uhalifu wa mitandaoni

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM) Mhandisi Mwanaisha Ulenge akihutubia Bunge la Dunia kupitia Jukwaa la Wabunge Vijana wa IPU linalofanyika nchini Bahrain. (Picha na mtandao).