Judith Ferdinand, Timesmajira online
Moja ya jitihada za serikali katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata haki ya msingi ya elimu ni pamoja na kuanzisha vitengo vya watoto hao kwa shule za msingi nchini.
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inatoa tamko kuwa Serikali itaendelea kuongeza fursa anuwai za elimu na mafunzo kwa usawa kwa makundi yote ya kijamii katika ngazi zote ikiwemo watoto wenye mahitaji maalumu.
Pia sera hiyo inatoa tamko kuwa Serikali itahakikisha kuwepo kwa miundombinu bora na stahiki ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Licha ya jitihada hizo za serikali za kuhakikisha watoto hao wanapata elimu kwa kuandikishwa katika shule mbalimbali lakini kumekuwa na changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa vifaa saidizi vinavyochangia kushindwa kuhudhuria masomo wakati wote.
Kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Igogo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali licha ya jitihada mbalimbali amabazo zimefanywa na serikali pamoja na wadau.
*Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Igogo azungumza*
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Igogo,Anthony Nelson, akizungumza na majira mara baada ya kukamilika kwa zoezi la utoaji wa vifaa saidizi kwa watoto wenye mahitaji maalum katika kitengo hicho vilivyotolewa na shirika la Plan International Aprili 25,mwaka huu shuleni hapo.
Anaeleza kuwa kituo hicho kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 40 wenye mahitaji maalum kati yao wavulana 23 na wasichana 17 huku walimu wakiwa ni watatu na wote ni wakiume.Mwl.Nelson anaeleza kuwa kituo hicho kilianzishwa Februari 2021, kikiwa na jumla ya watoto 28 kati yao wenye ulemavu wa akili wakiwa 21 wavulana 11 na wasichana 10,walemavu wa viungo 7.
“Kwa sasa kitengo kina watoto wenye ulemavu wa akili 30 kati yao wavulana 16 na wasichana 14,uziwi na usikivu hafifu wa 4, wavulana 3 na msichana 1,ulemavu wa viungo 8 wavulana 4 na wasichana 2,kuna jumla ya walemavu 40 kati yao wavulana 23 na wasichana 17,” anaeleza Nelson.
Changamoto kitengo cha watoto wenye uhitaji maalum Mwl.Nelson anaeleza kuwa moja ya changamoto inayowakabili katika kitengo hicho ni ukosefu wa darasa la kisasa lenye maliwato ndani yake ,hali hii husdabaabisha watoto kwenda kujisaidia mbali na chumba chao cha kujisomea.
Anaeleza kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa walimu wa kuwafundisha na kuwahudumia watoto hao wenye mahitaji maalum ambao ufindishwaji wao unahitaji uanagalizi maalum.
Pia anasema kuwa nje na vifaa katika ufundishaji wa watoto hao wanahitaji mwalimu mmoja afundishe wanafunzi watano na waliopo sasa ni walimu watatu ambao wote ni wakiume huku wanafunzi wakiwa 40.
“Kwa ufundishaji wa watoto hawa unahitaji muda wa kutosha na walimu wenye moyo maana wanahitaji kufundishwa huku wakihudumiwa au kusaidiwa kutimiza haja zao za msingi, ikiwemo haja ndogo hivyo,”anasema Mwl.Nelson na kuongeza kuwa
Pia mahudhurio hafifu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kutokana na ushirikiano mdogo kwa baadhi ya wazazi kuwaleta watoto wao shuleni,kwani hawaoni umuhimu wa kuwa shule kila siku.
Huku baadhi yao kutokana na uduni wa mazingira na maisha ya wazazi wao hivyo kushindwa kuwaleta shuleni kila siku hali inayochangiwa na ukosefu wa vifaa saidizi kwa ajili ya kuwasaidia kutembea na kufika shuleni kila siku.
“Watoto hao wanahitaji msaada wa kupelekwa shule ili wapate elimu na kurejeshwa nyumbani na wazazi wao au walezi kutokana na uwezo wao mdogo wa kuhimili mikikimiki ya barabarani lakini kutokana na baadhi ya wazazi kuwa na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao hutoa ushirikiano mdogo wa kuwapeleka shule na kufanya mahudhurio yao kuwa hafifu huku wakijikita katika utafutaji uchumi,”.
Ukosefu wa baadhi ya vifaa vya kujifunzia kama vile projecta,runinga na radio vinavyosaidia kuchangamsha ubongo wa watoto.
Vilevile amelishukuru shirika la Plan International kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum katika kituo hicho vifaa hivyo visaidizi ambavyo vitarahisisha katika kupata elimu.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa kitengo hicho hupokea fedha ya chakula toka serikali kuu kiasi cha zaidi ya laki tano,kila mwezi kuanzia Oktoba 2022 hadi sasa.
Mwalimu wa wenye mahitaji maalum shule ya msingi Igogo Gerald Manyilizu,anasema kuwa wanafundisha watoto mchanganyiko wa ulemavu wa viungo,akili, uoni hafifu (vipofu) usikivu hafifu (viziwi),changamoto katika kufundisha ni ukosefu wa vifaa vifaa saidizi vitakavyosaidia wakati wa kufundishwa.
Kwani watoto wenye ukiziwi wanahitaji kufundishwa kwa sauti kubwa na vitendo huku wenye upofu wanahitaji kusikia zaidi hali inayowawia vigumu kama walimu kuwafundisha watoto hao wenye uhitaji tofauti wa kufundishwa.
“Kutokana na watoto hao kuwa na mahitaji tofauti inampa changamoto mwalimu wa namna ya kuwafundisha,hivyo inamlazimu mwalimu kutumia muda mwingi katika kuwahudumia, kulingana na utofauti wa uhitaji kulingana na aina ya ulemavu,”.
Mwalimu huyo anashukuru kwa vifaa hivyo vilivyotolewa na shirika la Plan International ambavyo vinaenda kuwasaidia watoto hao kulingana na mahitaji yao.
*Wazazi wanena changamoto katika malezi ya watoto wenye mahitaji maalum*
Miongoni mwa changamoto inayowakabili wazazi hususani mama katika kuwalea watoto wenye mahitaji maalum na kushindwa kuwapeleka shule mara kwa mara ni kutokana na baadhi yao kutekelezewa familia na waume zao baada ya kuwazaa watoto hao.
Hivyo jukumu la kuwalea, kuwatunza, kufanya shughuli za nyumbani pamoja na kutafuta kipato cha familia kinabaki kwa mama hali ambayo anashindwa kumudu kumpeleka mtoto wake mwenye ulemavu shule kila siku kwani anahitaji mtu wa kumsaidia wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.
Mmoja wa wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum shule ya msingi Igogo Meresiana Deonise,anasema kuwa suala la kukimbiwa na mwanaume pindi unapozaa mtoto mlemavu ni jambo la kufikia maana anakunyanyapaa na wakati mwingine anaona kama unamtia nuksi kwenye familia.
Meresiana anasema kuwa yeye ni mama wa watoto wanne wawili wazima huku wawili walemavu akiwemo mwenye ulemavu wa miguu na ngozi ambayo imekuwa ikichanika chanika.
Anasema kuwa baada ya kuzaa watoto hao wenye ulemavu mwanaume alimkimbia na kuoa mwanamke mwingine hivyo majukumu yote ya kutunza familia yapo juu yake hali inayomuwia vigumu.
“Najishughulisha na biashara ndogo ndogo ya samaki ambapo uchumi wangu hautoshi kumudu mahitaji ya familia kwani mme wangu alinikimbia baada ya kuzaa watoto wenye ulemavu na kwenda kuoa mwanamke mwingine hivyo inasababisha mimi kushindwa kumpeleka mtoto wangu shule mara kwa mara,”anasema Meresiana na kuongeza kuwa
Sanjari na hayo changamoto nyingine inayowapa ugumu katika malezi ni hali ya jamii kuwanyanyapaa watoto wenye mahitaji maalum huku wengine kuwaona watoto hao kama watachafua nyumba zao pindi wanapoenda kwa majirani kucheza na watoto wenzao.
Vilevile ukosefu wa vifaa saidizi kwa ajili ya watoto wao kutumia kulingana na aina ya ulemavu walionao ikiwemo kiti mwendo inachangia sana wazazi kushindwa kuwapeleka watoto wao shule mara kwa mara kwani wengi wao wanatoka katika familia duni.
“Tunaishi kwa kumtegemea Mungu tu kwa sababu ni mtihani ambao tumeisha ipata na hatuna jinsi ya kuikwepa,nalishukuru sana shirika la Plan International kwa kumpa mwanangu kiti mwendo ambacho kitanisaiadia badala ya kumbeba mgongoni sasa nitatumia kiti hicho kumpeleka na kumfuata shuleni,” anasema Meresiana.
*Ombi kwa Serikali ili kufanikisha watoto hao wanapata haki yao ya msingi ya elimu*
Meresiana anasema kuwa ili watoto wao wenye mahitaji maalum waweze kupata elimu kama wengine wanaiomba serikali kutenga bajeti ya kununua magari kwa shule za umma kwa ajili ya wanafunzi hao ili kuwasaidia wazazi kuondokana na changamoto ya kutumia muda mwingi kuwapeleka na kuwarejesha nyumbani watoto hao.
Hali hiyo ambayo itasaidia wazazi hao kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli za uchumi ili kuweza kumudu mahitaji ya familia na kujiingizia kipato.
*Mchango wa wadau katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalum*
Katika kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali za kusaidia watoto wenye mahitaji maalum shirika la Plan International lilitoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa halmasahauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Ambapo jumla yao ikiwa ni wanafunzi 66 wakiwemo wa kitengo cha watoto wenye mahaitaji maalumu kutoka shule ya msingi Igogo Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Meneja wa shirika la Plan International Mkoa wa Mwaza Majani Rwahambali,akizungumza wakati wa zoezi la utoaji wa vifaa hivyo lililofanyika katika shule ya msingi Igogo,wilayani Nyamagana jijini Mwanza Aprili 25,mwaka huu.
Anaeleza kuwa wao kama wadau wanaunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora ikiwemo wenye uhitaji maalum.
Ambapo anasema miongoni mwa watoto wenye ulemavu wanashindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa vifaa saidizi hivyo kwa kushirikiana na serikali wameweza kutoa mchango wao kwa watoto hao kwa kuwanunulia vifaa hivyo.
Majani anaeleza kuwa wametoa vifaa hivyo saidizi vyenye thamani ya milioni 21 kwani serikali pekee haiwezi kumaliza na kutatua changamoto zinazowakabili watoto wenye mahitaji maalum katika kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu bila ya wadau mbalimbali kuwaunga mkono.
Ambapo kabla ya kutoa msaada huo waliwasiliana na mamlaka za kiserikali ikiwemo idara ya afya na elimu kisha kupita katika shule 40 ndani ya halmashauri hizo,kuwabaini watoto wanaoshindwa kufika shule au kufuatilia masomo kutokana na ukosefu wa vifaa saidizi.
Baada ya kuwabaini watoto hao wenye changamoto ya ulemavu waliwapeleka kwenye vipimo vilivyofanywa na na wataalamu wa afya ili kuweza kujua mahitaji halisi na kisababishi cha changamoto walizokuwa nazo ndipo wakato vifaa hivyo.
“Vifaa hivi tulivyotoa tulikubaliana baada ya kupata ushauri wa wataalamu wa kiserikali ikiwemo wa elimu na afya ndio waliotuelekeza vifaa gani vinavyohitajika kwa watoto kulingana na mahitaji walioweza kuyabaini wakati wa zoezi la kuwabaini watoto ha,” anasema Majani.
Pia anasema kuwa vifaa hivyo vitawanufaisha jumla ya watoto 66 kwa halmashauri zote mbili ambapo wametoa viti mwendo 32,vifaa saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye usikivu hafifu (shime sikio) 25,magongo 2,miwani 4, pamoja na vifaa kwa ajili ya watoyo wenye ulemavu wa ngozi.
Ambapo miongoni mwa shule hizo ni pamoja na shule ya msingi Igogo ambayo imepokea viti mwendo 4,vifaa vya masikioni (shime sikio) 5,miwani 3,pia katika shule ya msingi Buhongwa,Kayenze na shule nyingine zilizopo katika halmasahauri hizo.
“Tunafahamu kwamba kuna uhitaji mkubwa kwa watoto wenye mahitaji maalum waliopo hapa tutaendelea kufanya hivi kulingana na fedha tutakazokuwa tunapata,mwaka jana tumegawa vifaa kwa watoto 70 na kwa kipindi hiki ni watoto 66, kwa halamshauri zote mbili za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela,”anasema Majani.
Sanjari na hayo anasema kuwa shirika hilo limekuwa likishiriki katika shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na serikali na itaendeleza ushirikiano huo pamoja na jamii ambapo kwa sasa wanaendelea na ukarabati wa madarasa na ofisi mbili za walimu katika shule ya msingi Buhongwa.
Huku shirika hilo likisisitiza elimu jumuishi kwa wote ikiwa ni pamoja na watoto wenye ulemavu,wa kike na kiume,ili isifike mahali watoto wenye mahitaji maalum wakaachwa.
*Ofisa Elimu,Elimu Maalum Awali na Msingi Jiji la Mwanza anena*
Ofisa Elimu,Elimu Maalum Awali na Msingi Jiji la Mwanza,Zakiah Ahmed,anaseama halmashauri hiyo ina wafunzi wenye ulemavu 806 kati yao wavulana ni 447 na wasichana 359 wanaosoma elimu ya awali na msingi katika shule za msingi zenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum 44.
Zakiah anasema,serikali imekuwa ikishirikiana na mashirika mbalimbali kufanya juhudi kubwa za kutatua changamoto za kielimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Ambapo anasema awali kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza vitengo tisa tu ndio vilikuwa vinapata chakula lakini mpaka sasa ni shule 44 zenye watoto wenye mahitaji maalum vinapatiwa fedha ya chakula na serikali ikiwemo shule ya msingi Igogo.
Shule hiyo imeanza kupokea fedha hizo tangu Oktoba mwaka jana inayotolewa kila mwezi ambacho ni zaidi ya laki tano lengo ikiwa ni kuendelea kuwaondolea changamoto watoto hao.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani