December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujumbe wa EIB Global kutembelea Tanzania

*Kukutana na Rais Samia, Dkt. Mwinyi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

UJUMBE wa ngazi ya juu wa Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB Global), ukiongozwa na Makamu wa Rais wa benki hiyo, Thomas Ostros, kesho utatembelea Tanzania kwa ajili ya shughuli za kuimarisha uwekezaji nchini.

Ziara hiyo inatoa fursa ya kutathmini miradi inayoungwa mkono na EIB, hasa katika sekta binafsi, miundombinu ya umma, uwekezaji na kukuza uchumi wa bluu.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo utakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dt. Hussein Mwinyi pamoja na viongozi wa juu wa Serikali.

Mikutano hiyo itahusu makabidhiano ya awamu ya kwanza ya Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Ziwa Victoria. Uwekezaji wa EIB umeongeza wigo wa huduma za maji taka na maji usafi kwa wakazi wa mijini na pembezoni mwa miji ya Mwanza, Bukoba na Musoma.

Akizungumzia hilo Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB Global) Thomas Ostros amesema: “Uchumi wa Tanzania umeonesha ukuaji mkubwa katika miaka iliyopita. Serikali pia imeendelea kusaidia maendeleo ya sekta binafsi kwa kushirikiana na washirika wa ndani, kikanda na kimataifa.

“Hii imeifanya Tanzania kuwa mshirika mkuu chini ya mpango wa EU wa ‘Global Gateway’ na EIB. Tuna furaha zaidi kufanya kazi pamoja na washirika wetu nchini Tanzania ili kuimarisha zaid, sekta ya umma na binafsi,” amesema Ostros.

Naye Naibu Mkuu wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Emilio Rossetti amesema: “Ziara hii na mikutano inawakilisha ushirikiano wa kudumu wa Tanzania na “Team Europe” amesema.

Umoja wa Ulaya, Nchi Wanachama na mashirika yao ya utekelezaji na benki za maendeleo ya umma, hufanya kazi pamoja ili kutoa maono ya Global Gateway, kusaidia uwekezaji mahiri katika miundombinu bora, kuheshimu viwango vya juu zaidi vya kijamii na mazingira, kulingana na maadili na viwango vya EU.

Mazungumzo hayo pia yatahusu kazi zinazoendelea za ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vinavyoungwa mkono na EIB Global huko Bukoba, Kigoma, Tabora, Shinyanga na Sumbawanga.

Mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuchochea uwekezaji katika eneo hilo, kutengeneza ajira na hivyo kuongeza viwango vya mapato, kukuza biashara na maeneo jirani, kuvutia utalii na kuongeza mwingiliano wa kijamii na kiuchumi katika viwanja vya ndege.

Manufaa ya mradi huo pia, yatajumuisha ongezeko la usalama wa anga kwani viwanja vitano vitatii viwango vya kimataifa vya usalama.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa EIB Ostros atakutana na wawakilishi wa benki kuu nchini pamoja na baadhi ya wanufaika wa SME wa ushirikiano wa EIB Global na benki za biashara za ndani.

Mwaka jana, Tanzania ilikuwa mpokeaji mkubwa zaidi wa usaidizi wa EIB, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Nchi ilinufaika na EUR 270 milioni (TZS 777 bilioni) za uwekezaji mpya kusaidia biashara kote Tanzania kupitia ubia na Benki za Tanzania, ambazo ni CRDB, NMB na KCB-Tanzania.

Uwekezaji huo hadi sasa umewezesha kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati zaidi ya 10,000, kati yao zaidi ya 3,000 wanaongozwa na wanawake na zaidi ya 900 ni biashara za uchumi wa bluu na ushirika huko Zanzibar.

EIB ilianza shughuli zake nchini Tanzania tangu mwaka 1977 na tangu wakati huo ilitoa mikopo ya kufadhili miradi 36, ambayo ni Euro milioni 680 (karibu TZS 2 trilioni).

Lengo la EIB Global ni kuwekeza katika sekta zenye uwezo wa juu zaidi wa kuunda kazi endelevu, haswa katika kilimo, huduma za dijitali. Katika ziara yake hiyo, Ostros ametembelea baadhi ya wafanyabiashara waliopata msaada katika uchumi wa bluu Zanzibar, kwa kuzingatia wanawake na vijana.