November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uhalifu Arusha wapungua, Wastaafu waombwa kuwa mabalozi wazuri uraiani

Na Mwandishi wetu,Arusha

Mwenyekiti wa Usalama Wilaya ya Arusha Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Felician Mtahengerwa amesema uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa Jijini humo kutokana na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema hayo katika hafla iliyoandaliwa na Jeshi hilo kwa ajili ya kuwaaga wastaafu na kuwapongeza Askari waliofanya vizuri zaidi kazini pamoja na kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024.

Mtahengerwa ameongeza kuwa hali hiyo imetokana baada ya kufanya tathmini ya ulinganifu wa makosa ya kihalifu kwa mwaka 2022 ambapo imeonesha kupungua kwa makosa hayo kwa mwaka 2023.

Pia amebainisha kutokana na kupungua kwa matukio hayo, imepelekea Jiji hilo ambalo linapokea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kuendelea kufika kwa wingi katika Mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini huku akiliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha usalama wakati wote.

Kwa upande wake Nathaniel Kimaro ambaye ni mdau wa masuala ya ulinzi amelipongeza Jeshi hilo kwa namna ambavyo wameboresha mifumo ya kisasa ya kiulinzi ambayo imefungwa katika Jiji hilo ambayo itaenda kupunguza vitendo vya uhalifu, pia kuwabaini wahalifu halisi wanaofanya vitendo vya kihalifu katika jiji hilo.

Naye Stafu Sajenti Mstaafu wa Polisi (S/SGT) kwa niaba ya wasataafu wenzake ametoa wito kwa Askari wanaondelea na utumishi ndani ya Jeshi hilo kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa lakini pia akiwataka askari hao kumtanguliza Mungu na kumtegemea Mungu katika utendaji wao kazi na hatimaye kufika mwisho wa utumishi wao wakiwa salama.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP George Malema amewapongeza Wastaafu hao pamoja na Askari waliofanya vizuri kazini huku akiwataka Wastaafu hao kwenda kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya ulinzi na usalama katika jamii ili kuendeleza dhana ya Polisi Jamii ambapo amesema wao ni wanauzoefu wa kutosha katika maswala ya ulinzi.