January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchunguzi saratani ya mlango wa kizazi utawaokoa wanawake wengi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WANAWAKE wameshauriwa kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi mara kwa mara ili kuokoa maisha yao kwani Takwimu zinaonyesha wagongwa 68 kati ya 100 wa saratani wanapoteza maisha kutokana na kuhudhuria hospitali wakiwa katua hatua za mwisho za ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia afya, hasa afya ya uzazi, Marie Stopes Tanzania imesema Saratani ya mlago wa kizazi ni moja ya ugonjwa unaoongoza kwa vifo vingi zaidi duniani kote, ambapo Takwimu zinaonyesha katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa 76 wapya wa saratani ya mlango wa kizazi.

Katika kuadhimisha Siku ya Saratani ya Mlango wa Kizazi Duniani sambamba na siku ya wapendanao Shirika la Marie Stopes Tanzania litafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu juu ya saratani ya mlango wa kizazi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Pamoja na utoaji elimu Pia shirika litatoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti katika Hospitali ya Marie stopes Mwenge na vituo vyake vingine vilivyo Mwanza, Mbeya, Iringa , Zanzibar , Makambako- Njombe, Kimara- Dar es Salaam, Arusha , Musoma- Mara na Kahama- Shinyanga.

Ikumbukwe kuwa Kila ifikapo Februari 4,dunia huadhimisha Siku ya Saratani siku ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu masuala ya saratani ya mlango wa kizazi lakini pia kuhimiza watu kufanya uchunguzi kwani ugonjwa huo ukigundulika mapema kuna uwezo mkubwa wa mtu kupona au kupata nafuu kwa muda mrefu.