May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia awahakikishia wana-CCM, Watanzania maendeleo ya kasi na viwango

Na Penina Malundo,Timesmajira, Online

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Samia Suluhu Hassan amewahakikishia watanzania kuwa serikali anayoiongoza itaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa bidii, maarifa, nguvu na uaminifu wote ili kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo endelevu na kuinua ustawi wa maisha yao.

Pia amewataka watanzania kuunga mkono hatua hiyo kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa kwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri hali ya amani na kutambua kuwa jukumu hilo ni la watanzania wote.

Akizungumza leo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais Samia katika Uwanja wa CCM Karume, wilaya ya Musoma mkoani Mara katika kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

“Kwa Ujumla niwakumbushe Watanzania kudumisha hali ya amani na utulivu ili iendelee kutamalaki katika nchi yetu. Wakati tukifanya hivyo tukumbuke kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.”amesema Rqis Samia

Amewakumbusha wana CCM na Watanzania kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yao kwa sasa ni kuendelea na utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha miaka 5 ya mwelekeo wa sera za CCM 2020-2030 kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025. ikiwemo kukamilisha miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa pamoja na kuweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za kijamii.

“Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, usafiri wa anga, ujenzi wa bandari, usafiri wa baharini na maziwa makuu. Sambamba na kuendelea kujenga mazingira bora ya kutoa elimu, afya, kilimo na kuwawezesha wananchi kiuchumi,”amesema Rais Samia

Akizungumzia kuhusu Miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM,Rais Samia amesema safari ya Miaka 45 ndani ya Chama hicho haikua nyepesi kwa kuwa kimekuwa na ushindani wa vyama vingine vya siasa nchini ambavyo Mfumo wa demokrasia umepelekea CCM kufanikiwa na kuibuka na Ushindi kila msimu wa Uchaguzi unapofika.

“Ushindi huo unatokana na kujenga imani na kuongeza kuaminika na wananchi kutokana na msingi madhubuti wa imani ya Chama uliojengwa na waasisi wetu, pamoja na utekelezaji mzuri wa sera na ahadi kupitia ilani zetu za uchaguzi,”amesema Rais Samia

Amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kupima na kutathamini namna ambayo CCM imetimza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi wa Tanzania na namna ilivyoweza kuwa msaada kwa mataifa mengine.

Wakati huo huo Rais Samia alizindua rasmi matumizi ya kadi za kielektroniki ambapo Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Godfrey Chongolo alieleza kuwa malengo na madhumuni ya kuingia kwenye mfumo huo ni pamoja na kukiwezesha chama kuwa na mfumo wa kisasa wa kuweka na kutunza takwimu za wanachama wake, kusaidia chama kuongeza mapato yatokanayo na ada za uanachama wanaosajili sambamba na kadi hizo kuwapatia wanachama fursa ya kupata huduma mbalimbali zinazohusisha malipo ya kifedha na kuwa utambulisho wa wanachama.